
Idadi ya watu waliofariki katika ajali ya boti nchini DRC imefikia 143 kwa mujibu wa mamlaka wakati wengine kadhaa wakiwa hawajulikani walipo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Maofisa wanasema ajali hiyo ilitokea baada ya boti hiyo iliyokuwa imebeba abiria na mafuta kupinduka na kushika moto.
Mamia ya abiria walikuwa kwenye boti hiyo ya mbao kwenye Ziwa Kongo kaskazini-magharibi mwa DRC siku ya Jumanne wakati wa ajali hiyo, kulingana na Josephine-Pacifique Lokumu, anayeongoza ujumbe wa wabunge kwenye eneo hilo.
Ajali hiyo ilitokea karibu na Mji Mbandaka, mji mkuu wa Mkoa wa Equateur, kwenye makutano ya Ruki na mto mkubwa wa Kongo wenye kina kirefu zaidi duniani.
Kulingana na Lokumu miili 131 ilipatikana siku ya Jumatano, na mingine 12 ikipatikana siku ya Alhamisi na Ijumaa, Miili hiyo ikiwa imeteketea.
Lokumu aidha alieleza kwamba Moto ndani ya boti hiyo ulisababishwa na kitendo cha mwanamke mmoja, ambaye alikuwa ni abiria, kuamua kupika ndani ya boti hiyo, huku baadhi ya abiria, wakiwemo watoto na wanawake, wakitumbukia majini na kupoteza maisha kwa kusundwa kuongelea.
Hadi tukichapisha taarifa hii, haikuwa wazi ni abiria wanagapi walikuwa kwenye boti hiyo ila Lokumu alieleza kwamba ilikuwa na mamia ya abiria.
Ijumaa ya wiki hii, baadhi ya familia kwenye eneo hilo ziliripoti kukosekana kwa wapendwa wao waliokuwa kwenye boti hiyo na hakuwa na habari kuwahusu.