
Uongozi wa Tabora United jana usiku, Aprili 18, 2025 umetangaza kuachana na kocha Genesis Mangombe kutoka Zimbabwe kutokana na mwenendo usiovutia kwenye Ligi.
Na jana hiyohiyo ikamtangaza Simonda Kaunda kutoka Zambia kuwa mrithi wa nafasi iliyoachwa na Mangombe.
“Uongozi wa Timu ya Tabora United unapenda kumtambulisha Simonda
Kaunda raia wa Zambia kuwa kocha Mkuu kwa kipindi hiki cha kuelekea kumaliza msimu wa 2024/2025 Ligi kuu ya NBC soka Tanzania bara.
“Kaunda anachukua nafasi ya aliyekuwa kocha Mkuu Genesis Mangombe raia wa Zimbabwe ambaye tulisitisha mkataba wake kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kutokuwa na mwenendo mzuri wa matokeo.
“Kocha Kaunda mwenye umri wa miaka 33, amewahi kuvifundisha vilabu kama vile Nkana FC, Forest Rangers FC, Chambishi FC pamoja na Roan United FC zote za Nchini Zambia,” imesema taarifa ya Tabora United.
Mangombe anakuwa kocha wa tatu kuachana na Tabora United msimu huu akifuata nyayo za Francis Kimanzi na Anicet Kiazmak.
Chini ya Mangombe, Tabora Umepoteza michezo minne ambapo mmoja ni wa Kombe la Shirikisho la CRDB na mingine mitatu ni ya Ligi Kuu Tanzania Bara.