Mtiti wa lala salama Umeanza Championship

RAUNDI ya 27 ya Ligi ya Championship inaendelea tena wikiendi hii na baada ya jana kuchezwa michezo miwili, leo itapigwa mitatu katika viwanja mbalimbali kwa kila timu kutafuta pointi tatu muhimu, huku ikihitimishwa mingine kesho.

Kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, Bigman FC iliyochapwa bao 1-0, mechi ya mwisho dhidi ya Transit Camp, itacheza na African Sports iliyotoka suluhu na TMA ya Arusha, huku Stand United ‘Chama la Wana’, ikiwakaribisha maafande wa Green Warriors.

Stand United inaingia katika mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga ikitoka kuchapwa mabao 8-1 na Yanga Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya robo fainali, huku Green Warriors ikiichapa Geita Gold kwa bao 1-0.

Mchezo wa mwisho leo, utapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha na Mbuni FC iliyochapwa mabao 2-1 na Mtibwa Sugar itajiuliza mbele ya Transit Camp, yenye kumbukumbu nzuri baada ya kuichapa Bigman FC kwa bao 1-0.

Raundi ya 27, itahitimishwa kesho Jumapili kwa michezo mingine mitatu kupigwa na Geita Gold iliyochapwa na maafande wa Green Warriors bao 1-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu kucheza na Songea United iliyochapwa 2-1 na Stand United.

Mbeya Kwanza iliyoichapa Kiluvya United bao 1-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kucheza dhidi ya vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar yenye pointi 63, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuichapa Mbuni FC ya Arusha mabao 2-1.

Mchezo wa mwisho, utapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo TMA FC iliyotoka suluhu mechi yake ya mwisho na African Sports, itaikaribisha Kiluvya United yenye kumbukumbu mbaya ya kuchapwa bao 1-0 na Mbeya Kwanza.

Akizungumzia mwenendo wa ligi hiyo Kocha Mkuu wa Cosmopolitan, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’, alisema ushindani umekuwa mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu, huku akiweka wazi malengo yao kwa sasa ni kukipigania kikosi hicho kisishuke daraja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *