Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Stephen Wasira, amesema ni muhimu kwa wananchi kutambua kuwa ndani ya amani kuna haki, hivyo chama hicho kitaendelea kusisitiza umuhimu wa haki kwa Watanzania wote.
Wasira metoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 18, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara mjini Tabora akihitimisha ziara yake ya siku tatu katika mkoa huo.
Amesema baadhi ya watu, wakiwamo viongozi wa baadhi wa vyama vya upinzani wakiilalamikia kwamba CCM inahubiri zaidi amani bila kutenda haki, hususan wakati wa uchaguzi.
“Kuna wanaohoji kwa nini CCM inazungumzia amani lakini si haki. Wanaotoa hoja hizo ni watu wazito, lakini ni lazima wafahamu kwamba amani na haki haviwezi kutenganishwa. Amani ikikosekana, wanaoathirika zaidi ni wanyonge,” amesema Wasira.
Amesema sababu ya kufika Tabora, ni mahali ambako Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutoa machozi kwa ajili ya amani ya nchi.

“Amani ikivurugika, wanawake na watoto kutoka nchi jirani hukimbilia maeneo kama Tabora. Hivyo, tunapolinda amani, tunalinda haki ya wanyonge wasio na sauti,” amesisitiza Wasira.
Amesema kuna wanaojaribu kufanikisha mabadiliko ya Katiba kwa maslahi binafsi, wakihubiri haki kwa mtu mmoja badala ya haki ya wengi, jambo alilosema ni kupotosha dhana ya haki.
Akitolea mfano wa nchi jirani ambazo zimepitia machafuko, kiongozi huyo amesema amani ilipotea, haki za wananchi wengi zilitoweka na watu wao walilazimika kukimbilia Tanzania. “Sasa je, ikitokea hali kama hiyo hapa, Watanzania wataenda wapi?” amehoji.
Hivyo, amesisitiza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka utaratibu wa kuhakikisha haki inapatikana kupitia taasisi kama Bunge na Mahakama.
Amesema mtu anayehisi kunyimwa haki anapaswa kuitafuta kupitia njia hizo za kisheria, si kwa fujo au vitisho.
“Unasema utachoma nchi, kwa ruhusa ya nani? Hatutakubali mtu kuvuruga nchi kwa kutaka haki yake kwa nguvu. Hii ni kuvunja haki za wengine, hasa wanyonge,” amesema Wasira.
Amesema vitendo vya vurugu vinaweza kuathiri huduma muhimu kwa wananchi, kama vile kliniki zinazohudumia akina mama na watoto, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini wasishabikie maneno ya uchochezi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba ameonya kuwa chama hicho hakitasita kujibu propaganda za upinzani zinazolenga kuichafua serikali.
“Hatutasubiri viongozi wa kitaifa kuwajibu; tutaongea wenyewe,” amesema.

Wasira amehitimisha ziara yake mkoani Tabora kwa kukagua hali ya uhai wa chama, kusikiliza kero za wananchi, na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.