Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameonekana akizunguka katika nchi kadhaa za Afrika akimnadi Profesa Mohammed Janabi, anayewania nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika.
Mjumbe huyo maalumu wa Rais Samia Suluhu Hassan, mpaka sasa ameshazuru nchi 21 akiwa sambamba na Profesa Janabi, ikiwemo Congo Brazzaville, Niger, Guinea ya Ikweta, Burkina Faso, Ethiopia, Uganda, Cape Verde, Gambia, Algeria na Senegal.
Jana, Aprili 17, 2025, Kikwete alionekana jijini Ouagadougou nchini Burkina Faso alipokutana na Rais Captain Ibrahim Traoré. Katika nchi zote amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Katika nchi nyingine ikiwemo Malawi, Lesotho, Zambia na Zimbabwe waliowasilisha ujumbe huo maalumu ni Waziri wa Afya, Jenista Mhagama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Mchakato wa kumpata kiongozi wa WHO Kanda ya Afrika huhusisha kura moja kutoka mataifa 46 yanayounda bara zima. Kura hizi huamuliwa na kiongozi mkuu wa nchi husika, huku akiwakilishwa na Waziri wa Afya katika upigaji kura.

Hii ndiyo sababu Kikwete alikutana na Rais wa Burkina Faso, Traoré katika mkutano uliofanyika jijini Ouagadougou na kuhudhuriwa na maofisa waandamizi kutoka Serikali zote mbili.
Katika mkutano huo, Kikwete amesema, “Rais wangu amenituma nije kuwasilisha ujumbe maalumu kwako na nimefurahi umenipa fursa hiyo na leo umeupokea rasmi.”
Pamoja na hayo, Kikwete amewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais Samia kuhusu umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Afrika, hususan Burkina Faso na Tanzania, na kwamba anatamani kuona nchi hizo zikishirikiana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja Afrika iendeleze rasilimali zake.
“Miongoni mwa maeneo tunayoweza kushirikiana ni eneo la afya, hasa katika magonjwa ya moyo. Timu ya teknolojia ya Burkina Faso watakutana na Profesa Janabi leo (jana) na kuzungumza namna tunavyoweza kushirikiana katika eneo hilo na madaktari kuona namna gani tunaweza kufanya kazi pamoja,” amesema Kikwete.
Wadau wa afya wamesema kampeni za kimataifa, hasa za aina hiyo, si jambo rahisi. Hilo limethibitishwa na ujio wa wajumbe kutoka nchi nyingine kwa Rais Samia kuleta ujumbe maalumu.
“Mchakato wa kumpata kiongozi huyo unahusisha kura na wapiga kura ni viongozi wa afya, yaani mawaziri wa afya wa nchi wanachama 46,” amesema Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, na kuongeza:
“Marais wote wanawakilishwa kupitia mawaziri wao. Ukiwa na nia ya kufanya kampeni, kwa kuwa ni mambo ya kidiplomasia, kiongozi wa nchi ndiye anayehusika kumwombea kura mgombea wake. Kwa kiasi fulani mipango imeenda vizuri.”
Hata hivyo, amesema haijatumika gharama kubwa na hivyo ndivyo kampeni hufanywa. “Ujumbe utatumwa kwa Rais wa nchi husika. Rais anayemwombea kura mgombea wake hawezi kumtuma Katibu Tarafa, atamtuma mtu mwenye hadhi kufikisha ujumbe wake.”
Kwa upande wake, mtaalamu wa afya ya umma ambaye pia amewahi kufanya kazi WHO kwa miaka 10, Dk Ali Mzige amesema Tanzania imefanya kampeni kubwa kumnadi mgombea wake.
Hata hivyo, amesema Profesa Janabi anakabiliwa na kibarua kikubwa cha kujifunza namna ambavyo kazi zinafanywa WHO, ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa Dk Faustine Ndugulile.
“Atatakiwa kujifunza kwanza, tofauti na ilivyokuwa kwa marehemu Dk Faustine Ndugulile ambaye alishawahi kukaa katika kamati fulani za WHO,” amesema.
Tanzania itakavyonufaika
Miongoni mwa maswali yanayozunguka vichwa vya wengi ni kuhusu namna ambavyo Tanzania itanufaika, ikiwa Mtanzania atapata nafasi hiyo.
Miongoni mwa faida zilizotajwa ni kuingiza fedha za kigeni, pamoja na baadhi ya Watanzania kupata nafasi za kufanya kazi katika shirika hilo kutokana na mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika sekta ya afya.

Mafanikio hayo ni pamoja na miundombinu katika ngazi ya msingi, kupunguza vifo vya wajawazito na afya kwa wote. Hizo ni sifa zinazowezesha nafasi hiyo, ambayo ni mara ya kwanza kutolewa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Dk Mugisha amesema nchi itaingiza fedha za kigeni kupitia mishahara itakayopitia ofisi zake zilizopo Tanzania, ambayo ni mamilioni ya fedha. Hata hivyo, kiongozi huyo hawezi kwenda mwenyewe; wapo Watanzania waliowahi kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali ambao wanaweza kuambatana naye.
“Vifo vya uzazi asilimia 60 vinatokea Afrika. Ukiangalia sisi tumefanikiwa kupunguza kufikia 104 kati ya vizazi hai 100,000, lakini nchi kama Sudan Kusini bado vipo 1,100 kwa vizazi hai 100,000. Waliohusika kufanikisha haya wana nafasi kubwa ya kuambatana naye,” amesema Dk Mugisha.
Ametaja faida nyingine za kiutumishi, kwamba nchi itafahamu mengi yanayoendelea ndani ya shirika na itakuwa sehemu ya washiriki, hivyo kuongeza mchango wake Afrika na taifa litafaidika kwa kupata kazi, kandarasi na taarifa.
Pia amesema kuna mambo yatakayojitokeza katika uendeshaji wa shirika, kama nchi wanachama tutafaidika kwa kiasi fulani na miradi na mikakati inayowekwa.
“Kuna faida za kidiplomasia. Tuna fahari kuwa sasa tuna watu kama hao nje ya nchi kwa sababu Tanzania ina mchango wake mkubwa katika kuendeleza Afrika na ukombozi wa nchi mbalimbali. Huu ni wakati mwingine tunapata mtu ambaye atatuwakilisha kupambana na maradhi ya kuambukiza na yasiyoambukiza,” amesema.
Amehimiza kuwa faida nyingine ni kuwafungua vijana kwamba inawezekana kiongozi wa Afrika kutoka nchini kwake. Wengi wana sifa lakini wamekuwa hawaombi nafasi hizo.
Uchaguzi huo umeitishwa baada ya kifo cha aliyekuwa mteule wa nafasi hiyo, Dk Faustine Ndugulile kutoka Tanzania, aliyefariki dunia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.
Profesa Janabi ni nani?
Profesa Mohamed Yakub Janabi ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu mwaka 2022 hadi sasa. Ni mwanataaluma mbobezi katika sekta ya sayansi ya tiba akiwa na shahada tatu.
Ana Shahada ya Awali ya Udaktari wa Tiba (MD), Shahada ya Uzamili ya Udaktari (MSc) na Shahada ya Uzamivu katika Sayansi ya Tiba (PhD).
Ujuzi wake umeenea ndani na nje ya Tanzania kupitia kazi za kibobezi katika utafiti na tiba.
Aidha, Profesa Janabi ni Mhadhiri Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Magonjwa ya Moyo cha Marekani (FACC) na Mkaguzi wa matibabu wa usafiri wa anga aliyeidhinishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA-USA).
Kabla ya kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Muhimbili, Profesa Janabi alifanya kazi ya kibobezi katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ambako alikuwa Ofisa Mkuu Mtendaji kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2022.
Kuanzia mwaka 2005 hadi sasa, Profesa Janabi amekuwa daktari mkuu wa Rais Kikwete.
Nafasi nyingine alizonazo ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) kuanzia mwaka 2000 hadi sasa na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tiba cha South Carolina, Marekani kuanzia mwaka 2003 hadi sasa.
Ni mjumbe wa bodi kwenye taasisi kubwa za huduma ya tiba nchini zikiwamo Baraza la Muhas kuanzia 2022 hadi sasa, JKCI, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na Bodi ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Pia ni mtafiti na mwanasayansi mwandamizi wa majaribio ya chanjo ya Ukimwi (TaMoVac) kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 2002. Ni Daktari Mkurugenzi katika Shirika lisilo la kiserikali la Madaktari wa Afrika lenye makao yake Marekani.
Kwa miaka mingi ya utumishi wake kwenye tasnia ya sayansi ya tiba ndani na nje ya Tanzania, amehusishwa na tafiti nyingi na kufanikisha machapisho 83.
Chapisho la “Mtindo wa maisha na afya yako” ni juhudi binafsi za Profesa Janabi za kuhamasisha Watanzania kutambua jambo moja kubwa kuhusu afya zao: kwamba mtindo wa maisha ni kichocheo kikubwa cha ama kuwa na afya njema au kinyume chake.
Katika kitabu hicho ambacho ni mchango wake kwa jamii, anatoa elimu pana kuhusu mtindo wa maisha, ulaji wa chakula na uhusiano wake na magonjwa mengi yasiyoambukiza.
Profesa Janabi ni mume na baba wa watoto wanne. Anazungumza na kuandika vyema lugha kadhaa ukiachana na Kiswahili, anakijua Kiingereza, Kirusi na Kijapani.