Kibaha. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema kuanzishwa kwa bustani za wanyama ndani ya kambi za jeshi hilo ni sehemu ya kuongeza vyanzo vya mapato vinavyoweza kuboresha huduma mbalimbali na kupanua wigo wa ajira.
Baadhi ya kambi za jeshi hilo ambazo tayari zimeanzisha bustani za wanyama ni Mbweni iliyopo Dar es Salaam na Ruvu, Kibaha mkoani Pwani.
Mbali na faida ya mapato ambayo vikosi hivyo vinapata kutokana na viingilio kutoka kwa wateja wanaofika kutazama wanyama, pia, ni sehemu ya kutangaza utalii wa nchi hasa kwa wageni kutoka mataifa mengine.
Hayo yamebainishwa April 17, 2025 na Meja Jenerali Mabele, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa nyumba za kulala wageni ndani ya bustani ya wanyama inayomilikiwa na kikosi cha jeshi hilo katika kambi ya Ruvu, Kibaha mkoani Pwani.
“Kikosi cha Ruvu ni cha pili kuanzisha bustani ya wanyamapori, cha kwanza kikiwa cha Mbweni kilichoko Mkoa wa Dar es Salaam. Natoa wito kwa kambi zingine zenye nia ya kufanya hivyo zifanye kwani hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za mkuu wa nchi anapenda kutangaza utalii wetu,” amesema.
Amesema kuwa jeshi hilo lina majukumu mengi ikiwemo kuwapa ujuzi mbalimbali vijana unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa na taasisi zingine jambo linalochangia kupambana na umasikini.

“Miradi mbalimbali inayoanzishwa na vikosi vya jeshi hili inawasaidia vijana kujifunza kwa vitendo na pindi wanapomaliza mikataba yao wanatoka na ujuzi wa kufanya kazi mbalimbali,” amesema.
Mkuu wa Kikosi cha Ruvu JKT, Kanali Peter Mnyani amesema wamefikia hatua ya kujenga nyumba za kulala wageni ndani ya bustani hiyo ya wanyama kwa kutambua uwepo wa mahitaji hayo hasa kwa wageni kutoka nje ya nchi.
“Tumeendelea na maboresho ya bustani hii na kama mnavyoona nyumba zimekamilika, hivyo tutaanza kupokea wageni wanaokuja kufanya utalii hapa,” amesema.
Wananchi wanaoishi jirani na kambi hiyo wamesema kuwa kuanzishwa kwa bustani hiyo kutawapunguzia gharama ambazo awali walikuwa wanapata kwenda kuangalia wanyamapori katika mikoa ya mbali.
“Tumeletewa neema nyumbani, nikitoka Mlandizi hadi hapa, nauli ni Sh1,000 tu kwa bodaboda, naingia naangalia wanyama, naogelea kisha narejea nyumbani,” amesema Zuhura Mohamed, mkazi wa Mlandizi.
Kwa upande wake, Selina Mathayo amesema kuanzishwa kwa bustani hiyo kutaimarisha uhusiano bora baina ya wanajeshi na raia kwani awali baadhi ya wananchi walikuwa na hofu kuwa karibu na askari.

“Zamani wananchi walikuwa wanayaogopa sana majeshi, wanakuwa na hofu pindi wanapowaona wanajeshi, lakini kupitia mwingiliano wa sasa, tayari uoga unaondoka,” amesema.