Vita ya ndugu Ligi Kuu Tanzania Bara leo

Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea tena leo Ijumaa, Aprili 18, 2025 kwa mechi mbili zinazohusisha timu nne zilizo chini ya taasisi za kiserikali ambazo zitachezwa katika viwanja tofauti.

Mechi hizo zote mbili zitachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, timu mbili zilizo chini ya taasisi za ulinzi na usalama zitaumana ambazo ni wenyeji Tanzania Prisons dhidi ya JKT Tanzania.

Ni mchezo muhimu zaidi kwa Tanzania Prisons vile bado haipo salama kwenye msimamo wa ligi kwani ina pointi 24 na ipo nafasi ya 14 katima msimamo kulinganisha na JKT Tanzania iliyopo nafasi ya saba ikiwa na pointi 32 na imeshajihakikishia kutoshuka daraja moja kwa moja.

Katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam, timu mbili zilizo chini ya wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zitaumana.

Timu hizo ni wenyeji KMC dhidi ya Dodoma Jiji.

Ushindi ni muhimu zaidi kwa wenyeji KMC kwani wapo katika nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27 kulinganisha na Dodoma Jiji FC ambayo imeshakwepa kushuka daraja kutokana na pointi 34 ilizonazo.

Kocha msaidizi wa KMC, Steve Nyenge amesema kuwa timu yake imefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi hiyo.

“Tunaujua uzuri wa timu ya Dodoma Jiji na udhaifu wao. Lazima twende kwa tahadhari hivyo tutajilinda na kushambulia ili tuhakikishe tunapata matokeo mazuri,” alisema Nyenge.

Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema,”mchezo ni mgumu hivyo ni lazima tucheze kwa akili sana. Mechi zote ni fainali kwetu kwani kila mmoja anahitaji alama tatu muhimu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *