Askofu Kimario aishusha hadhi Parokia ya Ugweno, sababu yatajwa

Same. Jimbo Katoliki la Same limeishusha hadhi Parokia ya Ugweno iliyopo Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro kuwa kigango kwa madai waumini wake wameshindwa kuonyesha ushirikiano kwa Paroko wa kanisa hilo na kuifanya kazi yake ya utume kuwa ngumu.

Uamuzi wa kuishusha parokia hiyo kuwa kigango unatokana na uamuzi uliofanywa na Askofu wa jimbo hilo, Rogath Kimario, wakati wa adhimisho la misa takatifu ya sikukuu ya mapadri iliyoambatana na kubariki mafuta ya krisma iliyofanyika Aprili 15, 2025 katika Kanisa Kuu la Kristo Mchungaji Mwema, mjini Same.

Hata hivyo, jana kwenye mitandao ya kijamii ilisambaa taarifa ya Askofu Kimario kufanya uamuzi huo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na waamini wa parokia hiyo kutoonyesha ushirikiano na kushindwa kumhudumia Paroko wao, Padre Ernest Mkwizu, aliyekuwa akikosa mahitaji muhimu.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya kuishusha hadhi parokia hiyo, itaunganishwa na kigango cha Mavaanja na Kikweni ili kuunda parokia mpya ya Kikweni, ambayo itatoa huduma pia eneo la Vuchama, ambapo pia Padri Mkwizu ndiye atakayehudumu kama Paroko katika parokia hiyo mpya.

Hata hivyo, Mwananchi lilimtafuta mmoja wa mapadri aliyekuwa katika ibada hiyo, Savaltory Kisela wa jimbo hilo, ambapo alithibitisha taarifa hizo.

“Ni kweli Askofu Rogath Kimario ameishusha hadhi Parokia ya Ugweno kuwa kigango baada ya waumini kushindwa kumtunza Paroko wa parokia hiyo, na hii taarifa Askofu alizungumza wakati wa adhimisho la misa ya kuwekwa wakfu mafuta ya wakatukumeni, wagonjwa na krisma iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Same mjini,” amesema Padre Kisela.

Hata hivyo, taarifa hiyo imezua taharuki kwa waumini wa Kanisa Katoliki, ambapo baadhi yao wameonyesha kusikitishwa na taarifa hiyo.

Mmoja wa waumini, Crecensia Lucas, amesema kanisa linahitaji umoja na mshikamano ili kuiendeleza kazi ya Mungu, na kwamba pale waumini wanapolega kutimiza hilo ni kuwakatisha tamaa viongozi wa kanisa.

“Sijawahi kusikia kitu kama hiki, ndiyo mara ya kwanza, lakini moja la kujifunza ni kwamba waumini tunapaswa kushikamana na viongozi wetu wa kiroho wanaotuongoza ili tusiliangushe kanisa. Hawa waumini wa hili kabisa wanapaswa kujitafakari sana,” amesema muumini huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *