
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa kilianzishwa kama chombo mbadala kwa wanamageuzi, hivyo kipo tayari kumpokea mwanasiasa yeyote atakayetaka kujiunga nacho.
Sio kuwapokea tu, kimesema hata watakaotaka kugombea, watapewa nafasi kama wanachama wengine na kupitia michakato ya kikatiba ndani ya chama hicho.
Sambamba na hilo, ACT Wazalendo imeongeza muda kwa wanachama wake kuchukua fomu za urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani.
Hoja ya utayari wa kupokea wanachama ilianza kutolewa na Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).
“Kwa wale wanasiasa wanaotaka kufanya siasa, lakini milango imefungwa kwenye vyama vyao, wasivunje madirisha wala nyumba! Karibu ACT Wazalendo tufanye siasa.
“Tunaweza kuleta mageuzi tukiwa mchezoni. Uchaguzi ni jukwaa la kuelimisha na kuamsha umma (mobilization). Uchaguzi ni jukwaa la kuonyesha dunia tunachopigania,” aliandika Zitto Aprili 16, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo, jijini Dar es Salaam leo, Ijumaa Aprili 18, 2025, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amelieleza hilo akirejea historia ya ACT Wazalendo ilivyozaliwa na hatua za maendeleo ilizopiga zimejenga picha kwamba ilianzishwa kama chombo mbadala kwa wanamageuzi wasioridhishwa na mambo kwenye vyama vyao.
“Ukitazama kwa nini ACT Wazalendo ilizaliwa, ni kwamba ilizaliwa kuwa mbadala wa mambo yasiyoenda sawa,” amesema.
Amesema ndiyo maana hawakuona ajabu kumwona hayati Maalim Seif Sharif Hamad akihamia kwenye chama hicho baada ya kuona haridhishwi na mwenendo wa chama chake.
Kwa sababu hiyo, amesema haoni ajabu kusikia kuna wanasiasa wasioridhishwa na mwenendo wa mambo kwenye vyama vyao wanataka kujiunga na ACT Wazalendo.
“Niseme hadharani, mtu yeyote anayetaka kujiunga na ACT Wazalendo kwa nia ya kugombea au kutaka mabadiliko, tutampokea. Hatutasita, uteuzi iwapo atataka kugombea utafanywa kwa mujibu wa Katiba ya chama,” amesema.
Amesisitiza hilo, akilitaja kundi la G55 ndani ya Chadema linalopinga ajenda ya kuzuia uchaguzi, akisema wapo tayari kuwapokea.
“Kama wamechoka walipo, fursa ipo kupitia ACT Wazalendo,” amesisitiza.
Sambamba na hilo, ametangaza kuongeza muda wa kuchukua fomu kwa wanachama wanaotaka kugombea urais kupitia chama hicho, kuanzia sasa hadi Aprili 25, mwaka huu.
Kwa upande wa wanaoutaka ubunge na uwakilishi, amesema muda umeongezwa hadi Mei 31 na udiwani hadi Mei 25, na kwamba nafasi hizo ni kwa nafasi zote, zikiwemo za viti maalumu.
Nyongeza hiyo ya muda, amesema ni matokeo ya agizo la Kamati ya Uongozi Taifa katika kikao chake cha Aprili 15, mwaka huu visiwani Zanzibar.
Shaibu amesema hadi sasa waliochukua fomu za kugombea ubunge katika chama hicho ni 317, na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ni 106.
Amesema wamepokea ratiba inayokusudia kuandikisha wapigakura kwa awamu ya pili, na kwamba hilo litafanywa katika mikoa yote.
Ametaka Watanzania watumie fursa hiyo kwenda kujiandikisha na wasiyumbishwe na hoja kwamba wasiende kujiandikisha.
“Kitambulisho cha kupigia kura ndicho silaha namba moja ya kupambania thamani ya kura, kupigania demokrasia na kuikataa CCM.
“Mtu yeyote anayekwambia usiende kujiandikisha anakwambia uende kwenye mapambano bila silaha.Yeyote anayewahamasisha watu waikose silaha hiyo ya mapambano, anarudisha nyuma harakati za kupigania thamani ya kura,” amesema.
Amesema wanakwenda kuhamasisha nchi nzima na hawataki kubughudhiwa wala kusumbuliwa katika hilo.