Dodoma. Watanzania wametakiwa kudumisha amani na upendo hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani Taifa linahitaji umoja na mshikamano zaidi kuliko wakati mwingine.
Wito huo umetolewa Aprili 17, 2025 na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Kardinali Protase Rugambwa wakati akiongoza ibada ya Ekaristi Takatifu iliyofanyika Kanisa Kuu la Jimbo Kuu la Tabora.
Askofu Rugambwa amewataka Watanzania kushiriki siasa safi kwa kuepuka kelele, kutukanana na kubaguana kwa namna yoyote ile ili jamii iishi katika mazingira bora kwa furaha.

Askofu Rugambwa wa Jimbo Kuu Katholiki Tabora
Amesema huu ni wakati ambao wakristo na Watanzania kwa ujumla wanapaswa kushikamana katika kudumisha amani ya nchi kwa kutanguliza upendo kama Yesu Kristo alivyokuwa na upendo.
“Tunayafanya haya yote lakini tunapaswa kufanya zaidi hasa kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, wananchi wanapaswa kuliombea Taifa na ili tuweze kuvuka salama,” amesema Dk Rugambwa.
Hata hivyo, Askofu amesema siyo dhambi kwa watu wenye nafasi ya kushiriki siasa isipokuwa matendo na mienendo yao iendane na huruma na jinsi watakavyolijenga Taifa kwenye mshikamano.
Amesema katika mafundisho ya imani ni wajibu wa wananchi wote kwenda kuendeleza yale mema na kuondoa mabaya hasa katika siasa na uchumi ili kudumu katika upendo usiobagua kama ambavyo Yesu Kristo hakubagua hata wale wabaya.
Katika ibada hiyo iliyoambatana na tukio la kuwaosha miguu waumini, ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora.