Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelalamikia hali mbaya ya barabara za mikoa ya ukanda wa kusini, kikidai kama Serikali haitachukua hatua, zitaendelea kuchangia kuporomoka kwa uchumi wa maeneo hayo.
Mikoa iliyoko Kusini mwa Tanzania ni pamoja na Ruvuma, Njombe, Mtwara na Lindi.
Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuhusiana na malalamiko ya Chadema, amesema Serikali haijaisahau mikoa hiyo katika mipango yake ya maendeleo kama inavyodaiwa.

Msigwa amesema barabara muhimu inayotumika kusafirisha makaa ya mawe na mahindi kutoka Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma hadi Makambako mkoani Njombe tayari imeingizwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Barabara ya Songea hadi Makambako tumeshatangaza kuwa itajengwa kwa kiwango kipya cha lami. Barabara hii imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa kusafirisha makaa ya mawe kutoka Tanzania na hivi sasa inahudumia pia ukanda mzima wa Afrika Mashariki,” amesema Msigwa.
Amesema barabara hiyo itajengwa kwa awamu hadi itakapokamilika, lakini kwa sasa wameanza mchakato wa kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi wa reli kutoka Mtwara hadi Ruvuma, kupitia eneo la machimbo ya makaa ya mawe, ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo mizito.
“Daraja la Somanga mkoani Lindi kwa kweli ni changamoto lilianza kuharibika tangu mwaka jana, lakini tayari tumeandaa mradi mpya. Hatuwezi kuharakisha utekelezaji kwa sababu miradi hii inahitaji mabilioni ya fedha. Haiwezekani daraja likivunjika leo, kesho tu upate fedha haraka na kuanza kujenga upya barabara au daraja,” amesema Msigwa.

Leo Ijumaa Aprili 18, 2025, akizungumza akiwa Makao Makuu ya Mabaraza ya Chadema Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kusini, Aden Mayala, amesema: “Wananchi mara nyingine hujiuliza, hivi Serikali hii tumeikosea nini? Barabara zote za kuelekea Dar es Salaam kupitia Njombe pamoja na ile ya kupitia Lindi na Mtwara zimeharibika.”
“Juzi tu, daraja lililovunjika mwaka jana limevunjika tena na kwa wiki nzima lilikuwa halipitiki. Tunawaona viongozi kutoka Kusini wakisema marekebisho yatafanyika, lakini hadi lini?”
Amesema barabara ya kutoka mkoani Ruvuma kupitia Njombe nayo si nzima, ina viraka vingi. “Tukumbuke barabara hii inapitisha magari mengi makubwa yanayobeba makaa ya mawe, lakini pia kuchimba madini ya uranium na kusafirisha mazao mbalimbali. Tunajiuliza, sisi wa Kusini tumewakosea nini?” amehoji kiongozi huyo.
Ilichosema Tanroads
Mwananchi imezungumza na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta aliyesema Serikali imewapa Sh868 bilioni kwa ajili ya kujenga madaraja yote nchini yaliyoathiriwa na mvua za El Niño zilizonyesha mwaka jana, likiwamo daraja lilipo Somanga mkoani Lindi.
“Tumepata fedha hizo Sh868 bilioni kupitia mfuko wa dharura, na Mkoa wa Lindi peke yake kuna madaraja 13 yanajengwa, na haya yanayoendelea sasa ni kwa sababu mvua zimekuja vibaya, maji yakijaa yanakuja hadi site,” amesema Besta.
Amesema miradi yote inaendelea, huku akieleza mwenyewe hadi anazungumza na Mwananchi yupo Somanga kusimamia ujenzi wa daraja hilo, pamoja na timu yake hawajalala siku nne.
“Tutalijenga hili daraja na fedha zake zipo, na kinachosumbua kwa sasa ni hali ya hewa ya mvua zinazoendelea kunyesha,” amesema.

Kuhusu barabara ya Songea, Makambako mpaka Dar es Salaam, Besta amesema mkataba wake unatarajiwa kusainiwa hivi karibuni, na zaidi ya kilomita 100 zitajengwa kwa kiwango cha lami.
“Tunaendelea na kazi, na kwa kipande chenye changamoto kama Litukila tutakikarabati vizuri. Tunategemea miradi yote kukamilika hadi ifikapo Desemba mwaka huu, na kuna jumla ya madaraja 93 nchi nzima,” amesema Besta.