Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mwigizaji, marehemu Hawa Hussein (Carina), umewasili nchini leo Aprili 18,2025 ukitokea India ambako alikuwa akipatiwa matibabu kabla ya kufariki dunia.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mwili huo umesomewa dua kisha kupelekwa nyumbani kwao Magomeni Mapipa Mtaa wa Mvumi jijini Dar, ambapo utalala hapo mpaka kesho Aprili 19,2025 kisha utapelekwa kuswaliwa Masjid Maamur, Upanga na kupumzishwa katika makaburi ya Kisutu.
Carina alifariki dunia Aprili 15,2025 akiwa nchini India alikoenda kupatiwa matibabu ya tumbo ambalo limemsumbua kwa zaidi ya miaka saba, huku akifanyiwa upasuaji wa tumbo mara 26.

Februari 24,2025, Carina alielekea India kupatiwa matibabu baada ya kukamilika kwa taratibu za safari na gharama ya matibabu Sh54 milioni ambazo zilitokana na michango ya serikali na tasisi mbalimbali.

Utakumbuka Carina alionekana kama Video Queen kwenye wimbo wa ‘Oyoyo’ wa kwake Bob Junior lakini pia alicheza kwenye tamthilia ya kwanza ya mwigizaji Jacob Stephen ‘JB’ ya mwaka 2017 hadi 2018 iliyoitwa ‘Kiu ya Kisasi’.