
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Selemani Mwalimu ‘Gomez’ amesema licha ya kutokuwa na uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza, lakini anafurahi kuwepo katika timu inayokwenda kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kati ya Juni 16 hadi Julai 13 nchini Marekani na Wydad ni moja ya klabu nne za Afrika zitakazoshiriki sambamba na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Esperance ya Tunisia na Al Ahly ya Misri ambapo ilipata nafasi hiyo kwa ubingwa wa Afrika iliouchukua msimu wa 2021-2022.
Tangu ajiunge na wababe hao wa Morocco, Gomezs amecheza mechi moja kwa dakika 30 dhidi ya COD Meknes zilipotoka sare ya 0-0, ambapo bao alilofunga Mtanzania huyo lilikataliwa kwa madai alikuwa ameotea.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez aliyesajiliwa na timu hiyo katika dirisha dogo la mwaka huu akitokea Fountain Gate aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, alisema anajivunia kuwa sehemu ya kikosi kitakachoiwakilisha timu hiyo katika michuano hiyo, huku suala la kucheza akimuachia kocha.
Gomes ambaye aliondoka nchini akiwa kinara wa mabao akifunga sita kabla ya waliokuwa nyuma yake kuja kumpiku, alisema pamoja na kutokuwa na uhakika wa namba amekuwa akijifunza mambo mengi na kujijenga kiushindani.
“Unajua kupata tu nafasi ya kujiunga na timu hii kwangu ni fursa kubwa. Pia kitendo cha hii timu kupata nafasi ya uwakilishi kwenye michuano hiyo na jina langu likiwa miongoni mwa nyota wa kikosi cha Wydad ni mafanikio makubwa,” alisema Gomes na kuongeza:
“Nafurahia maisha ndani ya nchi hii, changamoto ya kukosa namba inaniongeza nguvu ya kupambana. Nashukuru nimekuwa nikipata walau dakika chache za kucheza hizo ninazozipata zinanipa nguvu ya kuonyesha kitu ili kulishawishi benchi liendelee kuniamini.”
Gomez akizungumzia maisha yake ndani ya timu hiyo alisema yanakwenda vizuri na kumpa nguvu ya kupambana kwani anaamini kuwa sehemu ya akiba kwa wachezaji wanaoanza kikosi ha timu hiyo pia kwake ni mafanikio kwa sababu timu hiyo imesheheni majina makubwa na nyota wengi wazoefu.
“Sina hakika ya namba, lakini nina uhakika wa kuwa sehemu ya timu inayocheza mechi husika na ukiangalia vikosi vya Wydad jina langu limekuwa likitokea mara nyingi nikianzia benchi na nimeshapata nafasi ya kucheza kwa dakika chache hii ni kubwa kwangu naendelea kuvuja jasho naamini nitatoboa.”