
Dar es Salaam. Halmashauri nchini Tanzania hazijajipanga kukabiliana na maafa, hususan mafuriko, kutokana na kutotenga bajeti maalumu kwa ajili ya shughuli hizo muhimu.
Hayo yamebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika ripoti yake aliyoangazia utekelezaji wa ukaguzi kuhusu usimamizi wa mafuriko, iliyofanywa kwenye halmashauri sita kwa miaka ya fedha 2020/21 hadi 2023/24, ikionesha ni halmashauri moja tu iliyotenga fedha kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa maafa.
Halmashauri nyingine tano, ambazo ni sawa na asilimia 83.33, hazikutenga rasilimali yoyote kwa ajili ya kuzuia na kujiandaa dhidi ya mafuriko.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ndiyo pekee iliyotenga fedha hizo, ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23 ilitenga Sh60 milioni na Sh10 milioni kwa mwaka wa fedha 2023/24. Halmashauri nyingine zilizotajwa ni Hanang’, Kilosa, Kinondoni na Mbeya.
Ripoti inaeleza, kwa ujumla, bajeti zilizotengwa kwa ajili ya uratibu wa shughuli za maafa ni ndogo, jambo linaloonyesha uzito mdogo unaotolewa na baadhi ya Serikali za mitaa katika kushughulikia athari za maafa kabla hayajatokea.
Amesema, kulingana na takwimu za mafuriko zilizopitiwa kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2023/24, mafuriko yamekuwa na athari tofauti za moja kwa moja na kusababisha vifo.
Hata hivyo, mwaka wa fedha 2023/24 kulitokea jumla ya vifo 130 vilivyosababishwa na mafuriko pekee. Pia inaonekana idadi ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko iliongezeka kutoka 64 mwaka 2020/21.
Kichere amesema, wakati wa mahojiano na maofisa wa Idara ya Usimamizi wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO-DMD), walieleza ongezeko la vifo lilitokana na kuongezeka kwa matukio ya mafuriko yaliyochochewa na mvua za El Niño zilizonyesha nchini kote kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi 2024, pamoja na janga la maporomoko ya tope lililotokea Hanang’ na kuua watu 89.
Licha ya kuongezeka kwa idadi ya vifo kutokana na mafuriko kwa vifo 66 mwaka 2023/24, sawa na asilimia 103 ikilinganishwa na vifo 64 vilivyotokea mwaka 2020/21, amesema ofisi ya Waziri Mkuu (PMO), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), na Halmashauri za Serikali za Mitaa (LGA), haikuchukua hatua za kuzuia majanga.
Amesema sababu mbalimbali zilitolewa na maofisa wa PMO na LGA kuhusu ongezeko kubwa la vifo vinavyotokana na mafuriko. Miongoni mwa sababu hizo ni uelewa mdogo na mwitikio wa taratibu kutoka kwa jamii zinazokaa kwenye maeneo hatarishi wakati wa juhudi za uokoaji na utafutaji wa manusura.
Pia, amesema kuna ukosefu wa uratibu wa kutosha miongoni mwa wadau wakuu wanaohusika na uokoaji wakati wa majanga ya mafuriko.
Amesema PMO-DMD ilieleza kuwa, kwa mujibu wa kifungu kidogo cha 31(2)(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, LGAs zilipaswa kutekeleza maagizo ya kujumuisha shughuli hizo kwenye mipango yao.
Aidha, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (PO-RALG) ilizikumbusha LGAs kujumuisha shughuli kama za kuzuia, kujiandaa, kukabiliana, na kurejesha hali baada ya maafa kwenye bajeti zao wakati wa mafunzo ya kujengea uwezo.
“Hata hivyo, ukaguzi haukuweza kupata ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa maagizo hayo yalizingatiwa, jambo linaloibua wasiwasi kuhusu utayari wa halmashauri hizo kukabiliana na majanga yanapotokea,” amesema CAG Kichere.
Changamoto nyingine kubwa iliyoibuliwa ni kutokuwepo kwa vifungu maalumu vya bajeti vilivyotolewa na Wizara ya Fedha kupitia Miongozo ya Mipango na Bajeti kwa ajili ya usimamizi wa maafa, hali inayofanya LGAs kushindwa kutenga fedha, hususan kwa maandalizi na kinga dhidi ya maafa.
Katika ziara ya ukaguzi uliofanyika kwenye halmashauri sita, ilibainika ni halmashauri za Rufiji na Kibiti pekee ndizo zilizoweza kutoa mafunzo kwa watendaji katika ngazi ya halmashauri na kata kwa mwaka wa fedha 2023/24, kwa kutumia mapato yao ya ndani.
Uwezo mdogo wa LGAs kutenga fedha kwa ajili ya usimamizi wa maafa, hususani katika maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko, umechangia ukosefu wa uelewa kwa jamii na mafunzo ya vitendo kuhusu namna ya kujiandaa na kujikinga dhidi ya majanga hayo.
Amesema matokeo ya hali hii ni kuendelea kushuhudiwa kwa athari kubwa za mafuriko, ikiwemo vifo, uharibifu wa mashamba, mali, na miundombinu kama barabara na majengo.
Wataalamu wa maafa wameshauri kuongeza msukumo katika kuziwezesha halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya maafa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vifungu maalum vya bajeti na kusimamia utekelezaji wa miongozo iliyopo.