


Ashira Girls Sekondari: Kutoka Foleni za Vyoo Hadi Darasa
la Kisasa
– Miundombinu Mpya
Yafungua Fursa
Na Mwandishi wetu , Moshi
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ashira, moja ya
shule kongwe katika Mkoa wa Kilimanjaro, sasa wanapumua kwa afueni baada ya
serikali kukamilisha ujenzi wa miundombinu mipya ikiwemo mabweni, madarasa na
vyoo.
Kwa miaka mingi, shule hiyo ilikuwa ikikumbwa na changamoto
ya msongamano katika mabweni na madarasa, hali iliyokuwa ikiathiri moja kwa
moja mazingira ya ujifunzaji.
Lakini hali hiyo imeanza kubadilika kwa kasi baada ya
serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni 269.7 kwa ajili ya utekelezaji wa
mradi wa kuboresha miundombinu shuleni hapo inayoendelea kuboreshwa ndani ya
kipindi cha miaka minne.
Akizungumza na Wnahabari , Dada Mkuu wa shule hiyo, Prisca
Saimon Baraka, alisema kuwa ujio wa madarasa na mabweni mapya umeleta
mabadiliko chanya katika maisha ya kila siku ya wanafunzi.
“Wakati najiunga na Ashira, tulikuwa tunabanana sana
mabwenini na kwenye madarasa. Lakini sasa kila darasa lina wanafunzi wachache
na mazingira ni rafiki kwa kujifunza. Hii imerahisisha kazi kwa walimu na
imetuongezea morali ya kusoma,” alisema Prisca.
Naye Belinda Ndosi, mwanafunzi wa kidato cha sita, aliongeza
kuwa hali ya awali ya msongamano kwenye vyoo ilikuwa ya kusikitisha.
“Kabla ya ujenzi huu, kulikuwa na foleni ndefu
chooni. Lakini sasa kila mtu anaweza kutumia choo kwa wakati na kwa heshima.
Tunaishukuru serikali, na zaidi Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali
elimu ya mtoto wa kike,” alisema Belinda.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Zainabu
Shushue, fedha zilizopokelewa zilitumika kujenga madarasa matano, choo chenye
matundu saba na bweni moja.
Miundombinu hiyo tayari imeanza kutumika na imeleta tija
kubwa katika kuboresha taaluma ya wanafunzi.
“Shule yetu ina jumla ya wanafunzi 820. Kupitia
mradi huu, tumeweza kupunguza msongamano na kurahisisha kazi ya ualimu, hasa
kwa wale wanafunzi wanaohitaji msaada wa ziada darasani,” alisema Bi.
Shushue.
Aliongeza kuwa shule inatarajia ongezeko la wanafunzi hadi
kufikia 900 mwaka 2025, hivyo ipo haja kwa serikali kuongeza mabweni zaidi ili
kukidhi mahitaji ya makazi ya wanafunzi wapya.
Wanafunzi wanasema miundombinu hiyo ni chachu ya mafanikio
na inaendana na dhamira ya taifa ya kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu bora
katika mazingira salama.
Ashira Girls Sekondari imekuwa ni miongoni mwa shule
zinazofaidika na juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia nchini kupitia miradi ya maendeleo ya sekta ya elimu.
The post ASHIRA GIRLS SEKONDARI :KUTOKA FOLENI ZA VYOO HADI DARASA LA KISASA appeared first on Mzalendo.