Umuhimu watoto kupimwa kisukari mapema

Wazazi wengi huzingatia kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo, hula vizuri, na kwenda shule. 

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo mara nyingi hupuuzwa, navyo ni vipimo vya sukari katika damu. 

Wengi hudhani kuwa kisukari ni ugonjwa wa watu wazima tu, lakini ukweli ni kwamba watoto pia wako katika hatari ya kupata ugonjwa huu, hasa aina ya kwanza ambao huanza utotoni.

Kisukari aina ya kwanza hutokea pale ambapo kongosho hushindwa kabisa kuzalisha insulini. Hali hii humlazimu mtoto kutumia insulini kila siku maisha yake yote. 

Tatizo kubwa ni kwamba dalili zake huwa za kawaida au kuchanganywa na magonjwa mengine. Kwa mfano, mtoto anaweza kuanza kukojoa mara kwa mara, kuwa na kiu isiyoisha, kula sana lakini bado kupungua uzito, au kuwa mchovu kila wakati. 

Wazazi wengine huchukulia hali hii kama uchovu wa kawaida au magonjwa mengine.Vipimo vya sukari huchangia kugundua hali hiyo mapema kabla ya kuleta madhara makubwa. 

Watoto wengi ambao hawagunduliwi mapema huingia hospitali wakiwa na hali mbaya sana inayojulikana kama DKA (Diabetic Ketoacidosis), ambayo ni hatari kwa maisha. 

Hali hiyo husababishwa na ukosefu mkubwa wa insulini mwilini, na mara nyingi husababisha kulazwa hospitali kwa dharura au hata kifo.

Aidha, watoto ambao wanatoka katika familia zenye historia ya kisukari, kuna umuhimu mkubwa wa kufanyiwa vipimo mara kwa mara. 

Kisukari si ugonjwa wa kuambukiza, lakini una uhusiano mkubwa na urithi. Hivyo basi, kama mzazi au ndugu wa karibu ana kisukari, mtoto yuko katika hatari zaidi.

Mbali na kugundua ugonjwa mapema, vipimo vya sukari vina faida nyingine nyingi. Kwanza, vinamfundisha mtoto kuzingatia afya yake. 

Mtoto anayejua umuhimu wa vipimo, huwa na uwezekano mkubwa wa kuzingatia maelekezo ya kitabibu, kujiamini, na kuishi maisha marefu na yenye afya.

Pili, vipimo huongeza uelewa miongoni mwa wazazi na jamii kwa ujumla. Kuna imani potofu kwamba kisukari ni laana au adhabu, jambo ambalo limechangia watoto wengi kuchelewa kufikishwa hospitali. 

Kupima sukari na kupata majibu halisi kutoka kwa mtaalamu wa afya husaidia kuvunja mitazamo hiyo potofu na kujenga jamii yenye maarifa sahihi.

Serikali,mashirika na wadau wa afya wana nafasi muhimu ya kuhakikisha huduma za kupima sukari zinapatikana hata katika maeneo ya vijijini.

 Vipimo hivi vinapaswa kuwa sehemu ya kawaida ya uchunguzi wa afya ya mtoto, kama ilivyo kwa upimaji wa uzito, urefu au chanjo. 

Aidha, kuna haja ya kuandaa kampeni za kitaifa za kuhamasisha wazazi kuhusu umuhimu wa kupima sukari kwa watoto wao, hasa wakati wa matukio ya afya ya shule au kwenye kliniki za watoto za kila mwezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *