Ripoti ya CAG mwanga wa uwajibikaji, ifanyiwe kazi

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/24, imeibua masuala mazito yanayoakisi udhaifu mkubwa katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Kupitia ukaguzi huo, CAG Charles Kichere amebaini kuwa Sh2.59 trilioni za tozo zilizokusanywa na TRA hazikupelekwa kwenye taasisi husika, hali inayoashiria ukiukwaji wa wazi wa sheria na Katiba ya nchi.

Aidha, upotevu wa mafuta na bidhaa zilizopaswa kwenda nchi jirani bila ushuru, umesababisha hasara ya zaidi ya Sh13.9 bilioni. Hali hii si tu kwamba ni fedheha kwa utawala wa sheria, bali pia ni pigo kwa juhudi za maendeleo ya Taifa.

Ni jambo la kusikitisha kuwa kila mwaka CAG amekuwa akitoa ripoti zinazobeba uzito wa makosa yanayojirudia bila hatua madhubuti kuchukuliwa kwa wakati.

Ripoti hizi hazipaswi kubaki kuwa nyaraka zinazosomwa kwa mbwembwe bungeni na kisha kuwekwa makabatini; badala yake zinapaswa kuwa nyenzo ya kuchochea uwajibikaji, ufuatiliaji na marekebisho ya kina katika taasisi za umma.

Mamlaka husika, ikiwemo Bunge, Wizara ya Fedha, TRA na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zina wajibu wa kuhakikisha kuwa mapendekezo ya CAG yanatekelezwa kwa dhati na si kwa matamko matupu.

Mfano kitendo cha Sh1.14 trilioni kutopelekwa kwenye mifuko husika kama ya maji, barabara, reli na umeme vijijini, ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hasa kwa maeneo ya pembezoni yanayohitaji huduma hizo kwa udi na uvumba.

Isitoshe, upotevu wa mafuta unaozidi lita milioni 14 na tofauti ya bidhaa zisizovuka mipaka zinaibua maswali kuhusu uadilifu wa wasimamizi wa biashara hiyo na udhaifu wa mifumo ya ufuatiliaji wa bidhaa.

Jambo hili linahitaji hatua ya haraka na siyo maneno ya kusuasua. CAG ameshatoa mapendekezo ya kisera na kiteknolojia, ikiwemo kuanzishwa kwa mfumo wa kufuatilia mafuta na bidhaa, lakini utekelezaji wake hauonekani kupewa kipaumbele.

Ni muhimu pia kuweka wazi kuwa taasisi zilizopata hati safi hazipaswi kujisifia pasipo kujitathmini upya. Kama alivyoeleza CAG, ndani ya hati hizo huenda kukawa na dosari ambazo hazionekani kwa juu juu.

Hii ndiyo maana ripoti ya CAG inapaswa kusomwa kwa kina na si kuangaliwa kama orodha ya alama tu, bali kama dira ya uboreshaji.

Kwa kuzingatia kuwa huu ni mkutano wa mwisho wa Bunge kabla ya uchaguzi mkuu, pendekezo la CAG la kujadili ripoti hiyo kwa haraka linapaswa kuungwa mkono.

Hakuna maana ya kuacha ripoti hii ife kifo cha mende, huku ikiwa na majibu ya maswali mengi ya kwa nini huduma muhimu haziwafikii wananchi.

Ni wakati sasa wa Serikali kuonesha kuwa ripoti ya CAG, zaidi ya taarifa, ni chombo cha mageuzi ya kiutendaji. Wale wote waliobainika na ubadhirifu wachukuliwe hatua, fedha zilizopotea zirejeshwe na mfumo mzima wa usimamizi wa fedha za umma upitiwe upya kwa jicho la kisasa.

Tukishindwa kuifanyia kazi ripoti hii, tutajenga utamaduni wa kuendeleza ubadhirifu, huku tukiwakatisha tamaa wananchi walioweka imani yao katika taasisi za umma. Ripoti ya CAG ni sauti ya dhamira ya taifa, na sauti hiyo lazima isikike, ifanyiwe kazi, na izae matunda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *