
Dar es Salaam, jiji kuu la biashara na lango kuu la kuingilia Tanzania, limekuwa likikua kwa kasi na kuvutia watu kutoka kona mbalimbali za nchi na nje ya nchi.
Kwa miaka mingi, jiji hili limekuwa kiashiria cha maendeleo na sura ya Taifa kwa wageni wanaolitembelea.
Hata hivyo, hali ya uchafu katika jiji hili ni aibu kwa Taifa na kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiafya.
Miji mingi duniani inatambua kuwa usafi ni sehemu ya ustaarabu. Jiji likiwa chafu, linaakisi taswira mbaya ya nchi nzima. Japo Dar es Salaam siyo mji mkuu wa kikatiba, lakini ni kioo cha Tanzania mbele ya wageni wengi.
Ndilo jiji la mabalozi, mashirika ya kimataifa, sekta ya utalii, na mikutano ya kimataifa. Hivyo basi, uchafu wa jiji hili siyo tatizo la eneo moja tu, bali ni doa kwa sura nzima ya Taifa letu linalosifika kwa sifa nyingi kimataifa.
Katika maeneo mengi ya jiji, taka zimekuwa sehemu ya kawaida ya mandhari. Barabara kuu, masoko, na hata maeneo ya makazi yamejaa taka ngumu na majitaka. Msimu wa mvua kama sasa jiji ndio kabisa halitamaniki.
Magari, hasa malori ambayo yanapaswa kuwa barabarani au kwenye yadi, sasa yameweka makazi ya kudumu mitaani.Kila eneo ni gereji au hifadhi ya magari katika jiji hili.
Mashimo ya taka hayafunikwi, na mifereji ya maji machafu imejaa taka zinazosababisha kuziba kwa mitaro, hali inayosababisha mafuriko hata kwa mvua ndogo.
Hii ni hatari kwa milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, homa ya matumbo na malaria. Hali hii si tu kwamba ni hatari kwa afya, bali pia inapunguza thamani ya maisha ya wakazi na kupunguza mvuto wa jiji kwa wawekezaji.
Kwa nini tumefika hapa? Kwanza, ni ukosefu wa elimu na uhamasishaji wa kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira.
Wakazi wengi hawana utamaduni wa kutunza mazingira, jambo linalosababisha kutupa taka ovyo, hasa katika maeneo ya wazi na mitaani. Na hilo linafanyika huku jiji likiwa limesheheni viongozi wa kiserikali na kisiasa.
Pili, miundombinu ya ukusanyaji taka ni duni. Katika baadhi ya maeneo ya jiji, magari ya taka hayafiki kabisa au hufika mara moja kwa wiki au zaidi, hali inayosababisha wananchi kuhifadhi taka majumbani au kuzitupa mtaani. Cha kushangaza zaidi, magari yenyewe nayo ni taka!
Tatu, usimamizi hafifu wa sheria za usafi. Sheria na kanuni zipo, lakini utekelezaji wake ni hafifu. Hii ni ishara ya udhaifu katika usimamizi wa sheria za miji.
Ili kukomesha aibu hii, mikakati madhubuti inahitajika; ni lazima kuwe na kampeni kubwa na endelevu ya kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa usafi wa mazingira.
Hii ifanywe kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, shule, na mikutano ya kijamii. Wananchi wafundishwe kuhusu athari za uchafu na wajibu wao binafsi katika kutunza mazingira.
Serikali za mitaa ziboreshwe kwa kupewa vifaa, rasilimali, na uwezo wa kutosha wa kuhakikisha taka zinakusanywa kwa wakati na kuchakatwa ipasavyo.
Magari ya taka yaongezwe, pamoja na kuanzisha vituo vya kuchakata taka kwa teknolojia ya kisasa. Kila mtaa uwe na utaratibu wa kudumu wa kuzoa na kuhifadhi taka kwa usalama.
Sheria za usafi zitekelezwe kikamilifu. Wanaotupa taka ovyo wapigwe faini au kuchukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria. Hii itasaidia kuwafanya watu waheshimu sheria na kuacha tabia ya kutojali usafi.
Aidha, ni muhimu kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi.
Hali ya uchafu haiwezi kutatuliwa na Serikali pekee. Kampuni binafsi na mashirika ya kijamii yahamasishwe kuwekeza katika usafi wa mazingira, kwa kudhamini kampeni za usafi au kushiriki katika uchakataji taka.
Nisisitize Dar es Salaam kuwa chafu ni aibu kwa Taifa. Hili ni jiji linalopaswa kuwa mfano wa kuigwa na miji mingine ya Tanzania. Ni mahali ambapo wageni wengi wa kimataifa hupita kwanza, hivyo linapaswa kuakisi sura halisi ya taifa letu: taifa safi, linalojali mazingira na ustawi wa watu wake.
Ni wajibu wa kila mmoja wetu, mwananchi, kiongozi, mfanyabiashara, na taasisi kuhakikisha kuwa jiji letu linakuwa safi na la kuvutia kila siku. Usafi ni ustaarabu. Dar es Salaam bila taka inawezekana!
Abeid Poyo ni mhariri wa makala wa Mwananchi. Anapatikana kwa simu: 0754990083