
Dar es Salaam. Wakati Wakristo leo wakiadhimisha mateso na kifo cha Bwana Yesu Kristo, wamekumbushwa kuwa na tumaini, upendo, umoja pamoja na mshikamano.
Akizungumza kuhusu siku hii alipozungumza na Mwananchi kwa simu, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini amesema Ijumaa Kuu inaadhimisha mateso ya Bwana Yesu Kristo aliyefariki kwa kumwaga damu.
“Kwa sisi Wakatoliki na baadhi ya madhehebu, hatuli nyama iwe ya aina yoyote siku hii, iwe ya ng’ombe, mbuzi au sungura.
“Ijumaa Kuu ni siku ya maombolezo. Kristo alikufa kwa ajili yetu ili tupate amani na upendo na kuwa kitu kimoja,” amesema.
Hivyo, amewakumbusha kutokula nyama kama ilivyo desturi ya siku hii, akisema sababu kuu ni kukumbuka mateso ya Yesu pale msalabani ambako alimwaga damu yake kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu.
Askofu Kilaini amesema ni kipindi cha kujinyima na kukumbuka mateso ya Bwana Yesu Kristo pale msalabani.
Akitoa ujumbe wake kwa Wakristo, Askofu Kilaini amesema kwa kuwa 2025 ni mwaka mtakatifu na dhima ya mwaka huu ni ‘Mahujaji wa Matumaini’, waamini na wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuwa na matumaini, licha ya kuzongwa na matatizo mbalimbali.
“Na ujumbe wangu kwa siku ya leo tunapoielekea Sikukuu ya Pasaka hapo Jumapili, watu wanapaswa kujitayarisha na kila mmoja awe wa haki na upendo ili dunia iwe ya haki na upendo,” amesema Askofu Kilaini.
Naye Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Clement Kihiyo amesema kanisa linaadhimisha Ijumaa Kuu ikiwa ni mateso na kifo cha Yesu Kristo.
“Kanisa liliweka utaratibu Ijumaa Kuu kufunga na kutokula nyama. Kwanza, nia ni faida ya kiroho: kutii agizo la Mungu na kujinyima kwa ajili ya kutoa kwa wahitaji.
“Kutokula nyama kwanza ni mapokeo ya tangu zamani kwamba mtu anapouawa kwa kumwaga damu, basi siku hiyo hawali nyama kwa tamaduni za Kiyahudi,” amesema na kuongeza;
“Pili, nyama ni kama fahari na ni gharama; hivyo Wakristo wanajinyima wale vitu vya kawaida waweze kutoa kwa wengine.”
Amesema katika siku ya Ijumaa Kuu kunakuwa na maombi yanayogusa nyanja zote za maisha.
“Pia tunatoa heshima ya juu kwa msalaba ambapo Kristo ndipo alipojitoa kwenye msalaba kuna wokovu, kwa hiyo mti wa msalaba ambao umemkomboa mwanadamu,” amesema.
Akitoa salamu za kuelekea Pasaka, Padri Kihiyo amewataka waamini wote wafufuke na Kristo katika siku hiyo, waache maovu waliyoyaacha kipindi cha Kwaresma bali waishi maisha mema yanayoipendeza Mungu na jamii nzima.
Padri Pascha Ighondo, kwenye chapisho lililoandikwa na tovuti ya Vatican, akielezea Msalaba wa Kristo, amesema ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu.
“Badala ya kashfa na utupu, msalaba unakuwa ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini.
“Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele.”
Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, yaani mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake.
Changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye.
“Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika fumbo la msalaba; mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo.”
Akieleza zaidi sababu ya kutokula nyama katika chapisho lililoandikwa na Mwananchi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Mtume wa Mwinjilisti jijini Dar es Salaam, Padri Revocatus Paul amesema Ijumaa Kuu ni siku inayotumiwa na waumini kutafakari wokovu uliokuja kwa njia ya msalaba.
Amesema katika siku hii Wakristo hawatakiwi kufanya shamrashamra kwa kile alichokitaja kuwa ni siku ya maombolezo ya kifo cha Yesu Kristo.
“Hatutakiwi kula nyama kwa sababu nyama ni ishara ya sherehe, na ndiyo suala ambalo waumini wanatakiwa walizingatie. Tunatakiwa kukaa kimya na kusali njia ya msalaba. Huo ni utaratibu wa Kanisa ulimwenguni, kuelekea Sikukuu ya Pasaka,” amesema Padri Revocatus.