
Dar es Salaam. Ukaguzi wa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), umebaini uwepo wa wafanyakazi 6,364 katika taasisi 43 wenye tarehe tofauti za kuzaliwa kati ya mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho (Nida) na mfumo wa mishahara.
Kwa mujibu wa CAG, kanuni za kudumu za utumishi wa umma za mwaka 2009 zinahitaji utunzaji sahihi wa kumbukumbu za watumishi wa umma, hivyo kutofautiana kwa taarifa kunadhoofisha uaminifu wa rekodi za wafanyakazi na kuathiri ufanisi wa taasisi katika kusimamia taarifa ya rasilimali watu.
CAG Charles Kichere amebainisha hayo katika ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Tamisemi, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2023/24 aliyoiwasilisha bungeni Aprili 16, 2025.
“Katika ukaguzi wangu, nilibaini wafanyakazi 6,364 katika taasisi 43 walikuwa na tofauti katika taarifa za tarehe ya kuzaliwa kati ya kumbukumbu za malipo katika mfumo wa usimamizi wa rasilimali watu na Nida,” amesema.
“Hali hii imesababishwa na makosa wakati wa kuingiza taarifa za watumishi katika mfumo wa usimamizi wa rasilimali watu, au kanzidata ya Nida kutofanya uhakiki wa kutosha wakati wa ukusanyaji na uhuishaji wa taarifa, au matumizi ya tarehe za kuzaliwa zilizokadiriwa badala ya zilizo kwenye vyeti rasmi,” amesema CAG Kichere.
Kichere amefafanua kuwa katika ukaguzi uliofanywa na ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23, ulibaini taasisi 184 zilikuwa na wafanyakazi 76,536 waliokuwa na kasoro hiyohiyo.
Hata hivyo, Kichere amesema kuwa pamoja na kuboreshwa kwa eneo hilo, juhudi zaidi zinahitajika ili kuondoa tofauti hizo na kuhakikisha kumbukumbu sahihi za watumishi zinatunzwa.
“Kutofautiana huku kunatia mashaka kuhusu usahihi na kuaminika kwa taarifa kuhusu tarehe ya kuzaliwa kati ya mifumo hii miwili, jambo linaloweza kusababisha makosa katika malipo ya mishahara, utambulisho usio sahihi wa wafanyakazi, na changamoto katika kukokotoa mafao ya wastaafu,” amesema Kichere.
Kutokana na hilo, CAG amependekeza Serikali ihakikishe taasisi husika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala), zinalinganisha taarifa za tarehe za kuzaliwa kati ya mifumo ya rasilimali watu na kanzidata ya Nida ili kuongeza ufanisi wa utendaji.
Makato makubwa kwenye mishahara
Katika hatua nyingine kwenye ukaguzi huo, CAG amebaini uwepo wa wafanyakazi 724 katika taasisi 22 wanaopokea mishahara halisi baada ya makato chini ya kiwango cha chini kinachotakiwa cha theluthi moja ya mishahara yao ya jumla, kutokana na uwepo wa makato makubwa kupita kiasi.
“Makato ya mshahara yanayozidi kiwango yanaweza kuwashawishi watumishi kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa manufaa binafsi. Pia yanaweza kushusha morali, hivyo kuathiri utendaji wao, ustawi na utoaji wa huduma kwa ujumla,” amesema.
“Napendekeza Serikali ihakikishe taasisi husika zinatekeleza udhibiti madhubuti ili kuzuia makato mapya yatakayosababisha wafanyakazi kupokea mishahara chini ya kiwango kinachokubalika,” amesema Kichere.
Miradi ya ujenzi 45 imekamilika, haitumiki
Mbali na hilo, katika ripoti hiyo, CAG amebaini kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 kuna miradi ya ujenzi 45 ya sekta za afya, elimu na utawala katika mamlaka 11 za Serikali za Mitaa yenye thamani ya Sh bilioni 5.64 iliyokamilika lakini haitumiki.
Kwa mujibu wa CAG, miundombinu hiyo haitumiki kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo upungufu wa watumishi, ukosefu wa samani, vifaa vya maabara za shule, na miundombinu mingine ya uendeshaji kama vile mahali pa kuchomea taka na vyoo.
“Kushindwa kutumia miundombinu iliyokamilika kutaathiri sekta za elimu na afya kwa kuchelewesha utoaji wa huduma, kunyima jamii manufaa yaliyokusudiwa na kusababisha uchakavu wa mali. Hali hii itaongeza gharama za matengenezo na hatari ya miundombinu hiyo kuchakaa kabla ya kutumiwa,” amesema.
“Nashauri kila mamlaka ya Serikali za Mitaa ihakikishe miundombinu iliyokamilika inatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, na kuhakikisha samani na vifaa vya maabara vinakuwapo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii,” amesema.