CAG abaini utata wa uendeshaji wa uwanja wa KIA

Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini uwepo wa utata katika uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), akitaka Serikali na mamlaka husika zitafute suluhisho la kudumu la utata huo.

Hayo yamo katika Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 uliofanywa na CAG na ripoti yake kuwasilishwa bungeni na kuwekwa katika tovuti ya ofisi ya Taifa ya Ukaguzi nchini.

CAG Charles Kichere amebaini KIA kwa sasa unafanya kazi chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) badala ya kufanya kazi chini ya Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (Kadco).

Kwa mujibu wa CAG, hii ni baada ya mkataba wa upangaji wa uendeshaji wa KIA chini ya Kadco kuisha muda wake Novemba 9, 2023.

CAG amefafanua kuwa Novemba 6, 2023, ikiwa ni siku tatu kabla ya muda wa mkataba kuisha, Wizara ya Uchukuzi iliandika barua ikielekeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kuchukua majukumu kamili ya kiutawala na kusimamia uendeshaji wa KIA mkataba utakapoisha.

Hata hivyo, Desemba 29, 2023, wizara iliandika barua nyingine iliyofuta maelekezo ya awali, na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Kadco kuendelea kutekeleza shughuli zake chini ya makubaliano yaliyopo hadi pale itakapotolewa taarifa nyingine kutoka serikalini.

Hii maana yake ni kubatilisha hatua ya TAA kuchukua madaraka kamili ya uendeshaji wa uwanja huo wa kimataifa.

“Utata huu unatokana na mawasiliano duni baina ya mashirika haya, kutokuwepo kwa mpango wa mpito wa wazi, pamoja na mfumo wa kisheria usio wazi,” ameeleza CAG katika taarifa yake, na kuongeza kusema kuwa:

“Hali hii inaleta changamoto katika uwajibikaji, hatari za udhibiti, changamoto za kimkataba kutoka kwa wadau, na hatari za kisheria kutokana na mkanganyiko wa masharti ya uendeshaji yasiyofafanuliwa vizuri,” amesisitiza CAG.

Amependekeza Wizara ya Uchukuzi ichanganue kwa ufasaha majukumu ya Mamlaka ya TAA na Kampuni ya Kadco ili kupata suluhisho la kudumu.

Sakata hilo bungeni

Aprili 2, 2024, suala la Kadco liliibuka kwa mara nyingine bungeni baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kusema KIA iko chini ya TAA na kuwa hakuna namna ambavyo Serikali itaweza kudharau ama kwenda kinyume na Bunge.

Novemba 2022, wakati wabunge wakipitia ripoti ya CAG, Bunge liliazimia uwanja huo uliokuwa chini ya Kadco, ukabidhiwe kwa TAA.

Hata hivyo, Novemba 2023, Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilirejea tena na jambo hilo bungeni, na Serikali ilitoa ufafanuzi kuwa kulikuwa na mkataba mmoja bado wa upangaji.

Novemba 10, 2023, Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Moshi Kakoso, walikwenda kushuhudia makabidhiano ya uwanja huu kati ya kampuni ya Kadco kwa TAA.

Hata hivyo, Machi 10, 2024, Kadco ilitoa siku 21 kwa wananchi 1,712 wa vijiji vinane waliovamia eneo la KIA kuondoka ili kupisha shughuli za uendelezaji wa uwanja huo, jambo ambalo ni miongoni mwa mambo yanayozua utata.

Akizungumza baada ya kipindi cha matangazo bungeni, Jumanne ya Aprili 2, 2024, Dk Tulia alisema baada ya makabidhiano hayo, Bunge lilimaliza kazi yake na masuala ya kiutendaji yanabakia kwa Serikali.

“Bunge haliwezi kufuatilia huko kung’ang’ania nani amefanya nini, nani amesaini barua gani; hiyo sasa tutakuwa tunaenda nje ya ule utaratibu tuliojiwekea wa mgawanyo wa majukumu na madaraka kwa mujibu wa Katiba,” alisema.

Dk Tulia alisema Machi 10, 2024 kulitokea changamoto, Kadco ilitoa notisi ya siku 21 kwa wananchi wahame kwenye eneo hilo.

Alisema changamoto ikajitokeza kwa kuwa barua hiyo iliandikwa na Kadco wakati Bunge na Serikali walishakabidhi kwa TAA, hivyo wangetarajia kuwa barua hiyo iandikwe na TAA na siyo Kadco.

Alisema kilichotokea ni suala la utendaji wa ndani ya Serikali na kwamba wao kama Bunge hawawezi kuingia huko kwenye utendaji wa Serikali, labda itokee changamoto.

“Kwa muktadha huo, ule mjadala uliokuwa unaashiria pengine Bunge limedharauliwa kwa Kadco kuandika barua, huo ni mchanganyiko pengine wa upande wa Serikali na sisi hatuingii katika utendaji. Lakini kwa upande wa maamuzi, Bunge lilishafanya,” alisema.

Alisema pia, Bunge lilishashuhudia kuwa uwanja huo umehamia TAA, hivyo Bunge linafahamu lilishafanya uamuzi kuhusu jambo hilo, na hakuna namna ambapo Serikali itadharau ama kwenda kinyume na maamuzi ya Bunge.

“Wabunge na wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu jambo hilo. Bunge lao linafanya kazi yake inayostahili, na Serikali inafanya kwa sehemu yake yale ambayo kikatiba wanapaswa kufanya,” alisema.

Dk Tulia alisema kama kutatokea changamoto, basi Bunge litashughulikia, lakini kwa sasa Serikali imepewa muda ikalifanyie kazi jambo hilo, na wanaamini watapata taarifa.

“Lakini kwa sasa hali iko hivyo. Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro uko chini ya TAA,” alisema Dk Tulia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *