Kilichotokea jana kwenye Uwanja wa Old Trafford kiliwakumbusha United yale maajabu waliyofanya mwaka 1999 kwenye Uwanja wa Nou Camp katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.

Ni miaka 26 imepita tangu yatokee maajabu yale ya Teddy Sheringham na Ole Gunnar Solskjær ambao waliwafanya mashabiki wa United washangilie kwa furaha. Sherringham alifunga bao la kusawazisha katika dakika 90 na baadae Ole Gunnar Solskjær akafunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi United ikanyanyua Kombe la UEFA.

Hivyo ndivyo mambo yalivyotokea jana pale Old Trafford ambapo Bruno Fernandes, Kobbie Mainoo na Harry Maguire walivyopindua meza kibabe baada ya kuwa nyuma kwa mabao 4-2 katika muda wa ziada (Extra Time).
Bruno Fernandes alifunga kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 114, Kobbie Mainoo akafunga bao la kusawazisha katika dakika ya 120 kabla ya Harry Maguire kufunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi.

Baada ya kupata ushindi huo Manchester United inatinga katika hatua ya nusu fainali kwa jumla ya mabao 7-6 huku ikitarajia kukutana na Athletic Club katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika Mei 1, mwaka huu, United ikiwa ugenini huku mchezo wa marudiano utachezwa Mei 8 kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Katika michezo mingine ilishuhudiwa Tottenham ikifuzu katika hatua ya nusu fainali baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Frankfurt. Tottenham itakutana na FK Bodø/Glimt ambao wameiondoa Lazio kwa mikwaju ya penati 2-3.

Katika mashindano ya Conference League, Chelsea ilisonga katika hatua ya nusu fainali kwa tofauti ya mabao 4-2 baada ya kupoteza mchezo wa jana kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Legia Warszawa kwani ilipata ushindi wa mabao 3-0 ilipokuwa ugenini.
Chelsea itakutana na Djurgårdens katika mchezo wa nusu fainali ambapo itaanzia ugenini Mei 1, 2025 kabla ya kucheza mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Stamford Bridge Mei 8.

Mchezo mwingine wa nusu fainali ya Conference League utawakutanisha Real Betis dhidi ya Fiorentina. Betis itaanzia nyumbani Mei 1 kabla ya kwenda ugenini kwenye mchezo wa marudiano Mei 8.