
Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amewataka Watanzania kuhakikisha mwaka 2025, wanatumia fursa za kidemokrasia kufufua matumaini ya kujenga nchi ya haki na kutetea wanyonge.
Fursa ya kidemokrasia inayozungumziwa na Askofu Bagonza katika mwaka 2025 ni Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, ukihusisha kupatikana kwa Rais, Wabunge na Madiwani.
Tayari vyama vya siasa vimepuliza kipyenga kwa wanachama wao kujitokeza kutangaza nia na kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali, huku Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pekee kikipanga kuuzuia uchaguzi huo, iwapo mabadiliko ya kisheria hayatafanyika.
Askofu Bagonza ameyasema hayo leo, Ijumaa, Aprili 18, 2025 katika ujumbe wake wa salamu za Sikukuu ya Pasaka 2025, alioutuma kwa Watanzania.
Katika ujumbe huo, amesema mwaka 2025 ni wa fursa katika taifa, akiwataka Watanzania wasiogope, badala yake watumie demokrasia kufufua matumaini ya kujenga nchi inayopenda haki na kuwatetea wanyonge.
Amewasisitiza kutumia fursa hiyo, ili kuepuka Serikali isigeuzwe kuwa gulio la kuuza na kununua haki za wanyonge.
“Tunaalikwa kuwa chachu ya haki iletayo amani katika taifa letu. Haki inatosha kuleta na kutunza amani. Tuukatae uzushi wa kuimba wimbo wa amani isiyotokana na haki,” amesema.
Kwa mujibu wa Askofu Bagonza kupitia salamu zake hizo, kifo cha Yesu kilibadilisha dhuluma kuwa haki, giza kuwa nuru, kilirejesha matumaini kutoka hali ya kukata tamaa.
“Yote matatu tunayo katika jamii yetu, dhuluma, giza na kukata tamaa. Kumbe basi, Yesu anatualika sote tuupokee ufufuko ili dhuluma iondoke na haki itawale, giza la mioyo lifukuzwe na nuru ya Kristo iangaze na waliokata tamaa wajazwe nguvu mpya,” amesema Askofu Bagonza.
Katika andiko lake hilo, Askofu Bagonza amekwenda mbali zaidi na kueleza, haijalishi utakufa kwa kutekwa, kuliwa na simba au mamba, bali Kristo amekupa uhakika wa hai na kukutana uso kwa uso na watesi na wauaji wako.
“Ikumbukwe Yesu Kristo hakupatikana na kosa lolote. Aliteswa na kuuawa ili kuwafurahisha wenye mamlaka. Furaha ya wenye mamlaka inayotokana na mateso ya wasio na hatia ni ya bandia na ya muda mfupi,” amesema.
Amesema wakati wa mateso ya Yesu, furaha ya watawala ilidumu siku tatu, mwenye haki akatoka kaburini, msamaha wa mfalme wakati wa sikukuu ulikwenda kwa jambazi.
Ameeleza Yesu hakuhitaji msamaha wa mfalme ili kutoka kaburini, alifufuka na yuko hai hata sasa.
Ametoa ujumbe wake huo akirejea maisha ya Yesu Kristo kwa mujibu wa imani ya dini ya Kikristo, aliyepitia mateso akafa, kuzikwa na hatimaye akafufuka na kwamba binadamu watauridhi uhai wake.
“Kwa kuwa sisi ni warithi halali wa kila kitu cha Yesu Kristo, basi tunarithi mateso yake na sasa anatuambia; tunarithi uhai wake baada ya kufufuka,” ameandika katika ujumbe wake huo.
Hata hivyo, amesema kufufuka kwa Yesu kunawakatisha tamaa wote wanaotumia na kutukuza kifo kama njia ya kuzuia mamlaka zao za kidunia zisihojiwe.
“Kufufuka kwa Yesu kunachochea watu wengi kukipokea kifo kama njia takatifu ya kurejesha haki katika jamii yaani, dhuluma inasulubiwa na haki inafufuka. Kwa kupigwa kwake, sisi tumepona,” linasomeka tamko hilo.
Wakati Bagonza akiyasema hayo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), linatarajiwa kuzungumzia mambo mawili ikiwa ni salamu za sikukuu hiyo.
Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa amesema hilo linatarajiwa kufanyika hivi karibuni.
“Kuna matukio kama mawili tunatarajiwa kuzugumza,” amesema Askofu Pisa bila kuweka wazi ni mambo yepi.