
Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ambaye ametia nia ya kugombea urais kupitia chama chake, amesema akipewa ridhaa atashughulikia mambo matatu mahsusi ili kuwasaidia Wazanzibar, ikiwemo kuwaunganisha.
Othman amebainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika nyumbani kwake Unguja, Zanzibar.
Amesema miongoni mwa mambo hayo ni kuguswa na maisha ya Wazanzibar ambao kwa muda mrefu wametengwa na watawala.
Tayari Othman amerejesha fomu ya kuomba uteuzi wa kuiwakilisha ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 katika nafasi ya Rais wa Zanzibar, akiwa mgombea pekee aliyetia nia kuwania nafasi hiyo kupitia chama hicho.
Othman aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar baada ya kifo cha mtangulizi wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki dunia Februari 17, 2021, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akizungumza kwenye mahojiano hayo Jumatano, Aprili 16, 2025 Othman amesema anakusudia kuwaunganisha Wazanzibar ambao wamegawanywa na watawala kwa maslahi yao, jambo linalorudisha nyuma maendeleo yao.
“Katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanza kwa vyama vingi, wananchi wa Zanzibar wamegawanywa bila sababu, na hii imeirudisha nyuma Zanzibar na kupunguza utendaji wa Serikali,” amesema kiongozi huyo.
Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, amesema hali ya kiuchumi ya wananchi ni mbaya licha ya fursa nyingi zilizopo, hivyo akipata fursa ya kuwa Rais wa visiwa hivyo, atahakikisha anatumia fursa zilizopo kuwainua wananchi kiuchumi.
Amesisitiza kwamba ataweka mkazo maalumu katika kuhakikisha vijana na wazee wanakuwa na shughuli za kufanya kuendesha maisha yao, badala ya kuwa tegemezi katika jamii wanamoishi.
“Wapo watu wana uwezo mkubwa wa kutengeneza samani, wengine wana uwezo wa kilimo na ufugaji, kuna fursa za teknolojia ya anga na bahari. Ukiwawezesha hawa, ukawanyenyua, lazima watawezesha na wengine.
“Suala la uwezeshaji wa wananchi si kurasimisha umaskini, siyo kuwasaidia rejareja kama inavyofanyika hivi sasa,” amesema Othman, ambaye aliwahi kuwa Mwendesha Mashtaka na Mwanasheria Mkuu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Jambo la tatu, Othman amesema atawawezesha Wazanzibar kunufaika na ardhi yao. Amesema ardhi ya Zanzibar ina thamani kubwa, lakini wananchi hawajanufaika nayo.
Amesema wananchi wanaoishi karibu na bahari, wamechukuliwa ardhi yao, bila kunufaika na ardhi hiyo.
“Kama Serikali imechukua ardhi ya mwananchi, kwanini asilipwe pesa, kwa sababu Serikali inapata hela nyingi kupitia biashara zinazofanyika kwenye uwekezaji kama hoteli? Mwananchi ashiriki katika uchumi, tumwezeshe,” amesisitiza Othman.
Mwamko wa Wazanzibar
Akizungumzia mwanamko wa Wazanzibar kisiasa, Othman amesema kihistoria, jamii ya Zanzibar na wananchi wake wana mwamko mkubwa hususani katika kushiriki masuala ya uchaguzi.
“Moja ya vitu ambavyo vimeweka rekodi Zanzibar ni turnout (kujitokeza) ya watu kwenye uchaguzi tangu mwaka 1961. Uchaguzi ambao haukuwa na watu wengi ni wa mwaka 1957, lakini uchaguzi wa mwaka 1961, 1963 na mpaka tumeanza chaguzi za vyama vingi, turnout imekuwa kubwa.
“Kwa hiyo, wananchi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa wanaelewa kwa sababu wanashiriki kwenye uchaguzi, isipokuwa kwa sababu ya yaliyotokea hapa katikati, watu wamepoteza imani na mfumo wetu wa uchaguzi, thamani ya kura yao imepotea,” amesema kiongozi huyo.
Hata hivyo, amekiri bado kuna kazi kubwa ya kuwahamasisha wananchi si tu kufahamu hatua za mchakato wa uchaguzi, bali pia kufahamu thamani ya kura zao katika kuleta mageuzi ya taifa lao.
Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo amesema wao kama viongozi hawawezi kusema hawana imani na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), bali tatizo lililopo ni kwa walio madarakani wanaitumia vibaya.
“Uchaguzi hauendeshwi na makamishna peke yake, unaendeshwa na sekretarieti. Sekretarieti ya Tume imejipambanua wazi kwamba wako pale kufanya kazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na si wananchi.
“Wanatafutwa kwa misingi hiyo, wanatekeleza kazi hiyo na bahati mbaya hata wanapofanya makosa, hawachukuliwi hatua. Sasa tunachosema, wala si kuwa na imani na tume ya ychaguzi, sisi hatuna imani na uongozi,” amesema Othman.
Ameongeza kuwa tatizo kubwa la Zanzibar ni kwamba imepoteza uongozi wa kitaifa ambao ungeweza kunyoosha mambo hayo.
Tathmini ya miaka mitano
Akizungumzia tathmini yake ya miaka mitano ya Serikali ya Zanzibar, Othman amesema imethibitisha kuwa watawala hawana imani na Wazanzibari.
Wanawaona hawatoshi kuijenga na kuiendeleza nchi yao, wanadhani wengine ndio wenye akili na uwezo kuwa serikalini.
“Sisi ACT Wazalendo, na mimi mahsusi, tuna imani asilimia 100 na Wazanzibari. Wawe wale wanaoishi ndani ya visiwa vyetu au nje ya visiwa hivi, Wazanzibari wana uwezo mkubwa sana. Lililo muhimu ni kuaminiwa na kushirikishwa.
“Ndio maana linapohusika suala la umoja wa kitaifa na maridhiano, sisi tunaamini kwa kina juu ya umoja wa Wazanzibari kwenye ujenzi wa nchi yao. Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa maridhiano ni njia mwafaka ya kupita kuelekea lengo la Zanzibar mpya,” amesema.
Umoja wa kitaifa
Akizungumzia mpango wa ACT Wazalendo kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Othman amesema chama chake kinapigania kuimarishwa kwa SUK, lakini upande wa pili hawako tayari katika hilo.
Amesema wamekuwa wakipigania SUK kama alivyosema Maalim Seif, kwamba; “SUK ndiyo chombo chetu, tukitumie vizuri kuelekea kwenye umoja wa kweli wa taifa letu la Zanzibar.” Amesema hiyo ndiyo dhamira yao wanayoipigania.
“Hii ndiyo njia ya kweli tunayoipigania, nchi iwe na umoja wa kweli wa kitaifa, isiwe mtu kutumia jukwaa hili kujihalalishia kuendelea kufanya uovu anaoutaka. Kwa hiyo, kwenye hilo, sisi hatuwezi na hatuna sababu ya kuvuruga umoja wa kitaifa,” amesema.
Kuhusu viashiria vya ushindi wanavyoviona, Othman amesema historia inaonyesha kura za upinzani zimekuwa zikiongezeka kila baada ya uchaguzi mmoja na mwingine tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.
“Viashiria vya ushindi viko vingi, waswahili wanasema ukiona mwizi anatafuta namna bora ya kujificha, ujue anafahamu kwamba mwenye mali yuko macho zaidi,” amesema Othman wakati akizungumzia suala hilo.
Kura ya mapema
Othman amesema msimamo wa chama chake ni kwamba suala la kura ya mapema hasa kwenye nafasi ya urais ni kinyume na Katiba, lakini watawala si watu wa kuheshimu hilo, hivyo wataendelea kulisimamia.
“Msimamo wetu ni kwamba tutaendelea kulisimamia hilo, tutashirikiana na wananchi na wale watu wenye busara ndani ya CCM kuhakikisha utaratibu huu ulioleta maafa mwaka 2020, unaondoka,” amesema Othman.