CAG aitahadharisha Bodi ya Kahawa soko la Ulaya

Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ametahadharisha uwezekano wa kukwama kwa upanuzi wa maeneo mapya ya kilimo cha kahawa kutokana na vikwazo vilivyowekwa katika mkataba wa Ulaya wa kuzuia uharibifu wa misitu.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimesaini mkataba wa Ulaya wa kuzuia uharibifu wa misitu duniani, ambapo CAG amesema endapo itabainika kukiuka mkataba huo inaweza kuwekewa vikwazo vya kutouza kahawa katika soko la Ulaya.

Katika taarifa ya ukaguzi kwa mwaka 2023/2024, mpango mkakati wa kuendeleza zao la kahawa kwa mwaka 2021-2025, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ililenga kuongeza uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani 300,000 kila mwaka ifikapo mwaka 2025.

CAG amesema kipengele cha 225 cha mkataba huo kinapendekeza hatua za kisheria zinazotaka uchunguzi kuwa unafanyika, uchunguzi unaoweza kusababisha kuwekewa vikwazo katika soko la Ulaya endapo itabainika uharibifu wa misitu unatokana na shughuli za uzalishaji za kilimo.

“Hii inatokana na msisitizo mkali uliowekwa katika kusimamia na kuzingatia matakwa ya mkataba huo, ambao malengo yake mama ni kuzuia uharibifu wa misitu na uoto wa asili,” amesema CAG katika ripoti yake hiyo inayoishia Juni 30, 2024.

“Uzingatiaji na utekelezaji wa matakwa ya mkataba huo, kwa namna nyingine unazuia jitihada za TCB na wakulima wa kahawa kuanzisha mashamba mapya ya kahawa kutoka katika maeneo ya misitu ambayo yanafaa kwa kilimo cha kahawa.”

CAG amependekeza TCB itumie mbinu bora na endelevu za kilimo kwa kutumia njia za kilimo ambazo hazikinzani na kanuni za kimataifa ili kupata soko katika masoko muhimu ya kimataifa, kuepuka vikwazo na kuwa na maeneo mbadala kwa kilimo cha kahawa.

Hii, kwa mujibu wa CAG, iende sambamba na kuongeza ufanisi wa mavuno ya kahawa kwa kutumia mbinu bora za kilimo ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji katika maeneo yaliyopo yanayolimwa kahawa kwa sasa.

Katika hatua nyingine, CAG amependekeza TCB kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, ihakikishe mahitaji ya sekta ya kahawa yanajumuishwa na kuzingatiwa kikamilifu katika Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo.

Pia, ametaka bodi hiyo iwe na mpango mbadala wa hatua za kuchukua kuimarisha bei ya kahawa endapo Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo utaendelea kuchelewa kuanza kutekeleza majukumu yake.

CAG ametoa mapendekezo hayo baada ya kubaini utekelezaji duni wa mkakati wa kuimarisha bei ya kahawa, ambapo TCB haijafikia lengo lake la kimkakati la kuimarisha bei ya kahawa lililoainishwa katika mpango mkakati wake wa miaka mitano.

Hii ilitokana na uamuzi wa Wizara ya Kilimo kuchukua jukumu la kuimarisha bei za mazao sokoni kwa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo, uliopewa jukumu la kusimamia uimarishaji wa bei za mazao kwa mazao yote ya biashara, ikiwemo zao la kahawa.

Hata hivyo, CAG amesema mfuko huo haujaanza kazi zake hadi sasa na TCB haijachukua hatua mbadala kushughulikia kuyumba yumba kwa bei ya kahawa sokoni, hali ambayo kwa kiasi kikubwa inaathiri uzalishaji wa zao la kahawa na sekta nzima ya kahawa.

Mpango Mkakati wa Bodi ya Kahawa ulilenga kusimamia na kudhibiti masuala yanayoathiri bei ya kahawa ili kuwa na udhibiti juu ya ubora wa kahawa na bei, anaeleza CAG katika ripoti yake hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *