Mshambuliaji amshtua kocha Stellenbosch

Kikosi cha Stellenbosch kimewasili leo tayari kwa pambano la kwanza la nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Simba, huku ikipata pigo.

Stellenbosch itavaana na Simba katika mchezo huo wa nusu fainali ya kwanza utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar

Kocha huyo amekiri kutomjumuhisha kikosini mshambuliaji muhimu, Ashley Cupido aliyeumia mapema wiki hii katika mechi ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).

Kukosekana kwa mshambuliaji huyo kunatokana na majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mchezo uliochezwa Jumanne dhidi ya Amazulu, huku Stellenbosch ikishinda bao 1-0 lililofungwa na Sanele Barns dk29.

Cupido ambaye alikuwa sehemu ya kikosi kilichoiondoa Zamalek katika hatua ya robo fainali kwa bao 1-0, amepata majeraha hayo dakika ya 10 tu tangu kuanza kwa mchezo huo dhidi ya Amazulu na kutolewa uwanjani kwa msaada wa machela, ikielezwa amepata maumivu makali yanayomfanya kuwakosa Simba.

Akizungumzia kukosekana kwa mshambuliaji huyo, kocha Barker amesema: “Ndio, inaonekana kama ni msuli mbaya wa paja, hakuna uwezekano wa kupatikana katika mchezo huo. “Tutafanya tathmini zaidi kujua ukubwa wa jeraha lake. Kiuhalisia majeraha hayo yanapotokea mchezaji anakuwa nje angalau wiki sita.

“Bahati mbaya kwake, pia ni bahati mbaya kwetu, ukizingatia kuwa Bradley Mojela bado yupo nje na sasa Ashley, ni dhahiri sio taarifa nzuri, lakini lazima tutafute suluhu.”

Kukosekana kwa Cupido, kumemwacha Barker na hali mbaya eneo la ushambuliaji kutokana na kuongezeka majeruhi mwingine baada ya Mojela ambaye anaendelea na matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti Desemba 2024.

Kutokana na hali hiyo, kocha Barker anazidi kuumiza kichwa kwani winga wake, Langelihle Phili anatakiwa kujiunga na kambi ya kikosi cha timu ya taifa ya Afrika Kusini chini ya miaka 20 kwa ajili ya kushiriki Afcon U20 nchini Misri, hivyo kuna uwezekano naye kumkosa.

Akizungumzia ishu ya Phili, Barker amesema: “Anatakiwa kuripoti kambini Jumapili, lakini tutamwomba asafiri nasi na kuripoti kambini siku ya Jumatatu ambayo tutakuwa tumerudi baada ya kutoka Tanzania. Kwa kuwa Ashley hayupo, tungeomba (Phili) aje kwa ajili ya mechi hiyo.”

Wakati huohuo, matumaini ya Barker ni kuona nahodha na kipa wa kikosi hicho, Sage Stephens atakuwepo kwa mchezo huo wa nusu fainali dhidi ya Simba kwani hakucheza mechi dhidi ya Amazulu kutokana na kupumzishwa baada ya kupata maumivu kidogo huku Oscarine Masuluke akichukua nafasi yake.

“Sababu ya kutocheza ilikuwa ni kumwacha apone kabisa. Kwa sasa anaonekana kuwa vizuri, hivyo atasafiri. Nina imani ifikapo wikendi atakuwa tayari kwa mechi. Msimu huu amekuwa mchezaji muhimu hivyo kuwepo kwake ni jambo zuri.”

Cupido amekuwa sehemu ya wachezaji muhimu wa kikosi cha Stellenbosch alichojiunga nacho msimu huu akitokea Cape Town Spurs ambapo amecheza mechi 21 za Ligi Kuu Afrika Kusini kati ya 23 na kufunga mabao matano huku akitoa asisti tatu.

Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, hajafunga bao wala kuasisti katika mechi tisa alizocheza kati ya 12.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Afrika Kusini, kikosi cha Stellenbosch Alhamisi hii kinatarajiwa kufika Dar es Salaam kisha kupanda boti kuelekea Zanzibar kutokana na ukosefu wa ndege ya moja kwa moja itakayowatoa Afrika Kusini hadi Zanzibar.

“Ni wazi tungecheza katika uwanja wenye viti 60,000 vilivyojaa labda vingetisha zaidi kuliko, tuseme uwanja wa viti 15,000 unatufaa,” alisema kocha Barker akiamini uamuzi wa mchezo huo kutolewa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kupelekwa New Amaan Complex, Zanzibar ni nafuu kwao.

“Nimeambiwa na kuona kwenye picha kwamba uwanja utakuwa katika hali nzuri sana, ni kweli lakini kuna safari ndefu ya kufika huko,” alisema kocha huyo.

Simba imelazimika kwenda kucheza Uwanja wa New Amaan Complex wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 15,885 baada ya serikali kuufungia kwa muda Uwanja wa Mkapa unaoingiza mashabiki 60,000 ambapo sasa unafanyiwa marekebisho kutokana na sehemu ya kuchezea kuonekana kuharibika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *