
Siku chache zilizopita, macho na masikio ya mstaafu wetu ambayo uzee wake sasa huyafanya yasione wala kusikia vizuri, pamoja na kupenda kwake kuyafagilia kuwa yameona na kusikia mengi yamemfanya kusoma na kusikia mengi.
Mengi hayo ni yale yanayoishia kupandisha shinikizo lake la damu na kuharakisha safari yake ya kuelekea Kinondoni kwa kasi zaidi ya G6 (kama ipo), na hakuna mheshimiwa yoyote anayeonekana kujali zaidi ya kuona ni drama zake tu mstaafu wetu.
Muungwana ‘Siaijii’ amefanya vitu vyake tena vya kuonyesha hela za siri-kali yetu, kwa maana hiyo za wananchi zinakopotelea.
Pamoja na waheshimiwa kutakiwa kulifanyia kazi haraka hili, mstaafu wetu anaishia kupandisha shinikizo lake la damu kama ilivyokuwa mwaka jana, mwaka juzi, na mwaka mtondogoo uliopita kwamba hakuna mheshimiwa yoyote wa taasisi na mashirika yaliyolitia hasara taifa aliyechukuliwa hatua.
Ni ‘Business as usual’, kisambaa kwa msisitizo. Ni kama vile hela hizo zinachukuliwa na majini au waruka na ungo wasioonekana, wanaochukua hela hizo na kulitia taifa hasara, pamoja na kwamba waheshimiwa wa taasisi na mashirika hayo yanayolitia hasara taifa wapo tu wanadunda.
Badala ya kuwataka wapumzike na kuwafilisi walichochuma kwa hela ya siri-kali, mbali na kuwataka wachape lapa na kuwaachia wengine wajaribu — hata kama hawajapitia VETA!Kwani wao wamepitia?
Mstaafu wetu hana haja ya kutaja mabilioni ya mapesa ambayo yameyeyuka kwenye taasisi zetu, ambazo nyingine tulizifungua kwa mbwembwe, lakini leo zinatia hasara taifa kama hazina akili nzuri zikiongozwa na siri-kali yenyewe, ambayo Muungwana ‘Siaijii’ amebainisha kuwa imepoteza mabilioni kadhaa ya shilingi kwa matumizi yasiyokuwa na maana yoyote.
Hapo ni pamoja na vitafunwa na kuwapeleka wasanii Korea kushangaa-shangaa, lakini siri-kali iliyaona ni muhimu zaidi kuliko nyongeza ya wastaafu na matibabu ya bure kwa wazee wa miaka 60 na zaidi — ndiyo maana waruka na ungo wasioonekana wameyayeyusha mabilioni hayo!
Mstaafu anaomba asizungumzie sana mabilioni haya kwa tarakimu, asije akawapa wastaafu wenzake shinikizo la juu la damu.
Ni dhahiri kuwa mabilioni hayo yameyeyushwa na ‘waruka na ungo’ wasioonekana, maana wangekuwa binadamu wanaoonekana wangechukuliwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yao na ‘Siaijii’ angekosa la kusema mwakani.
Anaomba pia asizungumzie hata deni la taifa, ambalo tuliishambiwa kuwa tukiendekeza sana kukopa kuna siku nchi yetu itauzwa!
Kuna hili linalomsumbua sana mstaafu, kiasi cha kuharakisha safari yake Kinondoni kuwa na kasi ya mwendo wa G6 (kama ipo): hili la kibubu chao cha akiba kuikopesha taasisi moja mabilioni kadhaa ili kujenga jengo la kufanyia biashara wamachinga miaka 17 iliyopita — na mabilioni hayo hayajarudi kwenye kibubu kwa miaka 17 sasa!
Mabilioni ambayo ni hela tuliyochanga wastaafu yanakopeshwa kwa mtu anayekaa nayo kwa miaka 17, akiwa amelipa shilingi milioni 20 tu ambayo haifiki hata robo ya deni lenyewe!
Tukumbuke kuwa hii si mara ya kwanza kwa kibubu cha akiba ya wafanyakazi kukopesha hela kwa taasisi kadhaa, bila wastaafu wenye hela zetu kukopeshwa kwa mtu bila kujua lolote.
Tukumbuke kwamba miaka miwili, mitatu iliyopita, wastaafu tulijua kuwa kumbe hata lile Daraja la Kigamboni hela zetu zilitumika na aliyezikopa alikaa na mkopo huo mpaka msamaria mwema mmoja alipoulipa. Kama aliulipa wote au bado deni halijaisha, tutajua mbele kwa mbele!
Kuna jambo linamchanganya mno mstaafu kuhusu kibubu cha akiba yao. Ni hela zetu wenyewe zilizokatwa kutoka kwenye mishahara yetu na kukianzisha kibubu hiki tulichokianza na ‘marehemu’ NPF — National Provident Fund.
Mstaafu hajui ni nani alianzisha utamaduni huu wa kibubu kuwa mkopeshaji bila hata kutuambia — tuliokianzisha kwa hela tulizokatwa kwenye mishahara yetu! Imezuka tu kwamba yoyote anaweza kukopa kwenye kibubu, kasoro mstaafu mwenyewe aliyekianzisha kwa hela yake!
Imefika mahali mstaafu wetu anadhani kuwa CV mojawapo kubwa ya ili mtu awe mheshimiwa wa kibubu ni yeye kuwa tayari kutoa mikopo kwa waheshimiwa wenzake wanapotaka mikopo bila ulazima wa kulazimika kwanza kutuuliza sisi wenye hela zetu.
Matokeo yake ndiyo haya ya kutoa mkopo na mtu anakaa na mabilioni yenu kwa miaka 17 na kulipa shilingi milioni 20 tu, wakati nyinyi mlioanzisha Kibubu mnapiga miayo tu!
Mstaafu ana wazo. Kibubu hiki tulichoanzisha wenyewe na sasa kinaelekea kimeota mapembe kichwani, sasa kuona siyo watumishi wetu tena bali waheshimiwa wetu, sasa kivunjwe. Rudia hapo, sasa kivunjwe na mashirika na taasisi zianzishe vitengo vyao vya kuhudumia wastaafu wa mashirika, kampuni, na taasisi zao.
Mstaafu wa TTCL akahudumiwe na kitengo cha wastaafu cha TTCL, wa Bandari akahudumiwe na kitengo cha wastaafu cha Bandari, wa Tanesco akahudumiwe na Tanesco, wa Siri-kali aende Siri-kalini — halafu wale wakopaji kisailensa waliozoea kukibamiza kibubu chetu sasa wakakope benki, halafu wakae na hela ya mtu miaka kibao, waone maana ya tozo!
Tulifanyie kazi. Sio tu kwamba tutapunguza tatizo kubwa la ajira nchini kutokana na vitengo hivyo kuhitaji wafanyakazi, tutakuwa tumedhibiti hii tabia ya kukopesha-kopesha hela za wastaafu wakati wenyewe hawana habari, wala hawapati faida yoyote na mikopo hiyo.
Mbali ya kwamba Kikokotoo na kuhakikiwa sasa kutabaki kuwa hadithi ya Alfu Lela Ulela! Unanihakiki vipi wakati tumefanya kazi shirika moja?