Askofu Sangu: Tudumishe upendo katika familia zetu

Shinyanga. Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu ametoa wito kwa waumini kudumisha upendo ndani ya familia zao, akisisitiza kila mtu hutoka katika familia na malezi ya mtoto hutegemea watu wanaomzunguka.

Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi Aprili 17, 2025, wakati wa Misa Takatifu ya Alhamisi Kuu iliyofanyika katika Parokia ya Buhangija, mkoani Shinyanga.

Katika ibada hiyo, Askofu Sangu ameosha miguu ya wazee 12, kama ishara ya kumbukumbu ya tendo alilolifanya Yesu Kristo siku kama ya leo.

“Tudumishe upendo katika familia kama Bwana Yesu Kristo alivyotupenda hadi kujitoa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu. Familia ni msingi wa elimu kwa kila mtu na mtoto hukua kulingana na malezi anayoyapata nyumbani,” amesema Askofu Sangu.

Ameongeza kuwa familia yenye upendo humfundisha mtoto moyo wa kujitolea, huku akionya kuwa familia yenye ubinafsi humlea mtoto mwenye tabia hiyo hiyo.

“Siku ya leo pia tunawaombea mapadri wote ili watimize majukumu yao kwa moyo wa upendo,” amesema.

Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki walioshiriki ibada hiyo wamesisitiza umuhimu wa kushiriki Ekaristi Takatifu, wakisema ni njia ya kumkaribia Yesu Kristo na kuimarisha moyo wa kujitolea.

“Kupitia mafundisho tunayopokea, tunaelewa kuwa mwili na damu ya Yesu vinatuunganisha na Mungu Mwana. Wakristo tusisite kushiriki Ekaristi Takatifu,” amesema Joseph Samson.

Kwa upande wake, Elizabeth John amesema “Wazazi tuwalee watoto wetu katika misingi ya kujitolea, iwe kwa fedha au matendo ya huruma,  ili kuwajengea tabia ya kuondokana na ubinafsi.”

Askofu Sangu pia ametoa mfano wa viongozi wa kitaifa waliowatanguliza Mungu katika maisha yao. “Tushiriki Ekaristi Takatifu kama walivyofanya hayati John Magufuli na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, waliomtanguliza Mungu katika kila jambo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *