Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amewataka Watanzania kutopuuza siasa, akisema ndio msingi utakaoboresha maisha yao.
Msingi wa kueleza hayo, umetokana na kile alichodai baadhi ya Watanzania wamekuwa mstari wa mbele kujadili na kufuatilia masuala ya mipira hasa klabu za Simba na Yanga badala ya siasa.
“Siasa ni maisha yako msipuuze, jadili mabadiliko ya maisha yako, ndio maana tumekuja kwenu mtuunge mkono katika hoja ya ‘No reforms, no election’. Mpo tayari kupigania kufa na kupona kuhusu Simba na Yanga, lakini hamko tayari kupigania siasa au kura yenu,” amesema.

“Tumekuja kuwaomba msipuuze siasa, kwa sababu mtateseka na maisha yenu hayatabadilika. Tusipopigania mabadiliko, sisi wenyewe badala yake tukaweka mbele muziki na Simba na Yanga, tutaendelea kuteseka,” amesema Heche.
Heche ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 17, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Tandika wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ukinadi ajenda ya ‘No reforms, no election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi), huku akisisitiza endapo wananchi wakiipuza siasa, nayo itawapuuza.
Operesheni ya ‘No reforms, no election’ imeanza Kanda ya Pwani Aprili 16, ikitarajiwa kukamilika Aprili 23. Tayari ‘No reforms, no election’ yenye lengo la kushinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi imeshafanyika mikoa ya Mbeya na Iringa.
Mikoa mingine ni Rukwa, Njombe, Songwe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Katika mkutano huo wa Temeke, Heche anasema ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kufanikisha mabadiliko ikiwemo kukataa mifumo mibovu ya uchaguzi isiyoruhusu haki kwa vyama vyote vya siasa.

“Tunachohitaji mfumo usiokuwa na upendeleo kwa mtu yeyote, ndio maana Chadema tunasema No reforms no election, kuwepo na tume huru yenye haki, tunahitaji kura yako iwe na heshima ili viongozi wawajibike kwako,” amesema.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Ali Ibrahim Juma amesema chama hicho kimeamua kwa dhati kabisa kuwasimamia Watanzania kupata haki zao za msingi kupitia ‘No reforms, no election’.
Juma amesema ni wakati wa kuungana ili kudai mabadiliko waliyoanza yatakayotoa fursa kwa wananchi kura zinazopigwa zinaheshimiwa na kiongozi wanayemtaka anapatikana kwa kutangazwa ili kudumisha amani.
“Tunaamini mifumo ikiwa safi Chadema kitashinda nafasi nyingi na kwenda kuwatetea Watanzania kwenye nafasi za maamuzi, tofauti na mfumo uliopo sasa si rafiki na tukisema tuingie kwenye uchaguzi yatajitokeza ya mwaka 2019, 2020 na 2024,” amesema Juma.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema Tanzania imejaliwa na utajiri mkubwa wa rasilimali na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alitoa wosia ili nchi ipige hatua kimaendeleo inatakiwa kuwa na mambo manne.
“Kwanza alisema watu wakati huo tulikuwa milioni saba (7), pili alisema ardhi na tunayo kubwa na inafaa kwa kilimo, tatu siasa safi na uongozi bora, lakini tunachoamini Chadema tumekosa uongozi bora ndicho kinatusumbua kama nchi,” amesema Lyimo.
Lyimo amedai tangu kupata uhuru mwaka 1961 Watanzania wengi ni maskini na haujaletwa na Mungu, bali chimbuko lake ni kukosa viongozi wasiokuwa na ufikiri mkubwa kuweza kuzitumia rasilimali zilizopo na kuwanufaisha watanzania wote.
“Tuna kila sababu ya kuweka uongozi wenye maono ili kubadilisha maisha ya Watanzania, umaskini wetu haujaletwa na Mungu tunatakiwa kupata watu wa kutuvusha na kufikia maisha tunayostahili kuishi,”amesema Lyimo.