
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu ni hitaji la lazima na siyo hiari tena.
Waziri Ulega ametoa kauli hiyo katika harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya mkutano wa Kimataifa wa Elimu Mtandao ( E-learning Afrika ) utakaofanyika nchini Mei 7 hadi 9 mwaka huu.
Harambee hiyo iliyofanyika jana usiku Aprili 16, 2025, iliandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Ulega alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Dotto Biteko.
Kupitia harambee hiyo, taasisi mbalimbali zimechangia Sh1.56 bilioni, zitakazotumika kugharamia kongamano hilo.
“Katika Karne ya 21 mahitaji ya teknolojia yameongezeka kwa kiasi kikubwa na matumizi ya teknolojia ya kidigitali siyo hiari tena bali ni hitaji la lazima na msingi kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu bora, jumuishi na ya kisasa,” amesema Ulega na kuongeza;
“Ndiyo maana sera ya elimu imeboreshwa na imesisitiza matumizi ya teknolojia na ubunifu na kubiasharisha teknolojia hizo tusiwe soko tu.”
Pia amesema kongamano hilo amblo linafanyika nchini, litawakutanisha mawaziri zaidi ya 50 watakao jadili na kuazimia mikakati ya kuzalisha nguvu kazi mahiri katika matumizi ya teknolojia Afrika.
“Ni heshima kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa kongamano hili na kutokana na fursa zinazoambatana na mkutano huu, Rais Samia ameridhia kuwa mgeni rasmi na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi atakuwa mgeni wakati wa kufunga kongamano hili,”amesema.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Carolyne Ndombo amesema kongamano hilo la kimataifa la 18 la elimu mtandao hii ni mara ya pili linafanyika nchini.
Amesema mkutano huo utawakutanisha washiriki 1,500 na mawaziri zaidi ya 50 akidokeza kupitia kongamano hilo, Tanzania itapata mbinu na mikakati ya kuongeza matumizi ya kidigitali nchini.
Mbali na hayo, amesema Tanzania itauza bunifu za teknolojia zilizobuniwa nchini pamoja na kuvutia kampuni za teknolojia kikanda na kimataifa kuwekeza nchini.
Fursa nyingine aliyoisema ni kuvutia kampuni za teknolojia kikanda na kimataifa kuwekeza nchini.
“Kongamano hili litachagiza uchumi wa ndani kupitia bidhaa na huduma za ndani zitakazotolewa na washirika wa kongamano, pia titakuza utalii, hili ni kongamano kubwa na tutanufaika na fursa nyingi,” amesema.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo; “Kufikiria upya elimu na maendeleo ya rasilimali watu kwa ustawi wa Afrika” linafanyika kwa mara ya pili nchini, kwa mara ya kwanza lilifanyika mwaka 2011.
Amesema kupitia kongamano hilo kufanyika nchini ni kielelezo cha diplomasia ya Tanzania kukua na itanufaika kwa kubadilishana mawazo na mataifa mbalimbali.