
Baada ya kujitokeza kwa kasoro ya eneo la kuchezea (Pitch) kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema eneo hilo halikuwa sehemu ya ukarabati unaoendelea.
Amesema eneo hilo lilikarabatiwa mwaka 2023 na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kwa ajili ya michuano ya Chan ambapo ukarabati huo ungedumu kwa miaka miwili.
Awali uwanja huo ulifungiwa na Caf kutokana na dosari za eneo la kuchezea baada ya ukaguzi uliofanyika siku chache tangu kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara iliyowakutanisha Simba dhidi ya Azam iliyochezwa Februari 24, 2025.
Baada ya kufungiwa na CAF, siku chache baadaye ukafunguliwa na kuipa nafasi Simba kucheza dhidi ya Al Masry, mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya robo fainali, Aprili 9, 2025, ndipo ikaibuka dosari nyingine sehemu ya kuchezea na Serikali kuamua kuufungia kufuatia kujaa maji yaliyotokana na mvua kubwa kunyesha siku ya mchezo huo.
Akizungumza leo Aprili 17, 2025 kwenye warsha ya wadau wa Utamaduni na Sanaa, Msigwa amesema kwenye mechi ya Simba dhidi ya Al Masry eneo la kuchezea limeonekena limepoteza uwezo wa kuondoa maji kwa haraka na si kuondoa maji kabisa.
Amesema tayari wameleta wataalamu kutoka Uturuki watakaoungana pamoja na waliopo nchini kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo kwa muda mfupi na uwanja uweze kutumika kwa michuano ya hivi karibuni ya kimataifa.
“Caf walikarabati kwa ajili ya michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi ya Ndani (Chan) ambayo ingechezwa Septemba 2024 na baada ya hapo ungekarabatiwa tena, lakini ikahamishiwa Februari mwaka huu na sasa wamesogeza hadi Agosti, tunaona muda umeongezeka,” amesema Msigwa.
“Baada ya michuano ya Chan Agosti, tutafanya matengenezo makubwa wa eneo la kuchezea kwa kuondoa sehemu ya juu na tutapanda nyasi mpya, lakini kwa sasa hivi tutafanya matengenezo ya kutumika kwenye michuano hiyo,” amesema.
Msigwa amesema mwishoni mwa mwezi Aprili uwekaji wa viti utakuwa umekamilika kutokana na makubaliano yao na mkandarasi ambapo shughuli hiyo ilikuwa ya mwisho.
Amesema ufungaji wa viti ni sehemu ya programu ya mkandarasi na shughuli hiyo ilikuwa ni ya mwisho vikiagiwa viti 62,000 na tayari vimefika 40,000.
“Hadi leo ameshafunga viti 20,000 na ukarabati umefikia asilimia 80 na kazi inaendelea, pia tumeamua viti viakisi rangi ya bendera ya Taifa na sehemu ya zege kuna ‘material’ wanaweka ili uwanja uweze kuvutia,” amesema.