
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekipa siku 21 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwasilisha mahakamani utetezi wake wa maandishi katika kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali na uendeshaji, inayokikabili.
Kwa maana hiyo chama hicho kimeamriwa kuwasilisha mahakamani hapo utetezi wake huo kabla au mpaka kufikia Mei 9, 2025.
Amri hiyo imetolewa leo Alhamisi Aprili 17,2025 na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo, wakati ilipotajwa kwa mara ya kwanza.
Kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye anajitambulisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha ni wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa chama hicho.
Wamefungua kesi hiyo, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mdaiwa wa pili.
Kesi hiyo ilipoitwa, mawakili wa wadai, Shaban Marijani ameieleza mahakama kuwa tayari wameshawapatia wadaiwa nyaraka za kesi hiyo.
Mawakili walioiwakilisha Chadema, Jeston Justine na John Chogomo wamekiri kupokea nyaraka hizo na wakaiomba Mahakama iwape muda wa siku 21 kuandaa na kuwasilisha utetezi wake, kwa mujibu wa sheria.
Wakili wa wadai, Marijani amesema kuwa hana pingamizi dhidi ya ombi hilo na Jaji Mwanga pia akaridhia.
“Maombi ya upande wa wadaiwa yamekubaliwa na wanapewa siku 21 kutoka leo (Aprili, 17,2025) kuwasilisha utetezi wake. Hivyo wadaiwa mnaelekezwa kuwasilisha mahakamani utetezi wenu kufikia au kabla ya Mei 21, 2025”, amesema Jaji Mwanga.
Pia Jaji Mwanga amepanga kuwa kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 12, 2025, kwa ajili ya kuangalia kama maelekezo hayo yatakuwa yamekamilika na kwa ajili ya amri nyingine muhimu.
Katika kesi hiyo wanaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.
Wamechukua hatua hiyo na kuomba Mahakama iamuru na kutamka hivyo wakidai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa msingi huo, walalamikaji hao wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaiomba Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Amri nyingine wanazoomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika.
Mbali na amri hizo, vilevile wanaiomba Mahakama iamuru , wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.