Man United, Spurs katika mechi za mtego leo

Usiku wa leo Aprili 17, 2025, macho ya mashabiki wa soka yataelekezwa kwenye viwanja mbalimbali barani Ulaya ambako hatua ya robo fainali ya michuano ya Europa League na UEFA Conference League itaendelea kwa mechi za marudiano.

Katika michuano ya Europa League, Manchester United itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Olympique Lyon kwenye Uwanja wa Old Trafford. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Ufaransa, na sasa United watalazimika kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani ili kusonga mbele.

Kocha wa Man United, Ruben Amorim amethibitisha kuwa kipa André Onana ataanza, licha ya makosa aliyoyafanya wiki iliyopita. United wanahitaji kufanya vizuri katika michuano hii ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwani msimu huu wamekuwa na wakati mgumu kwenye Ligi Kuu wakishika nafasi ya 14.

Mchezo mwingine utawakutanisha Athletic Bilbao dhidi ya Rangers kwenye Dimba la San Mamés, baada ya kutoka sare tasa kwenye mchezo wa kwanza. Bilbao wana kiu ya kufika fainali kwani mwaka huu uwanja wao ndio mwenyeji wa fainali ya Europa League.

Eintracht Frankfurt watachuana na Tottenham kwenye Uwanja wa Deutsche Bank Park. Frankfurt wanajivunia rekodi nzuri wanapokuwa nyumbani, wakati Spurs wakikumbana na changamoto ya matokeo mabaya waliyokutana nayo ugenini katika michezo ya hivi karibuni jambo linalowafanya wenyeji kuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele.

Kwa upande wa UEFA Conference League, Chelsea watawakaribisha Legia Warsaw kwenye Uwanja wa Stamford Bridge katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya UEFA Conference League. Baada ya ushindi wa 3-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Poland, The Blues wana nafasi nzuri ya kusonga mbele huku kocha Enzo Maresca akitarajia kutumia mchezo huu kuimarisha kikosi chake hasa baada ya matokeo yasiyoridhisha katika Premier hivi karibuni.

Katika Dimba la Artemio Franchi, Fiorentina ya Italia watakuwa na kazi nyumbani dhidi ya NK Celje ya Slovenia. Mechi ya kwanza iliisha kwa sare ya bao 1-1, na sasa kila timu inaingia kwenye mchezo wa marudiano ikiwa na matarajio makubwa ya kusonga mbele.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Jagiellonia ya Poland ambao watawakaribisha Real Betis ya Hispania. Real Betis walishinda mabao 2-1 katika mechi ya kwanza, Jagiellonia wana kazi ya kufanya kuhakikisha wanapindua matokeo na kusonga katika hatua ya nusu fainali.

Ratiba Europa League

Eintracht Frankfurt vs Tottenham Hotspur

Lazio vs Bodø/Glimt

Athletic Club vs Rangers

Manchester United vs Lyon

Ratiba UEFA Conference League

Jagiellonia Białystok vs Real Betis

Fiorentina vs NK Celje

Chelsea vs Legia Warszawa

Rapid Wien vs Djurgårdens IF

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *