Polisi Dar yapiga ‘stop’ kusanyiko Kisutu Aprili 24 kesi ya Lissu

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeonya wananchi kutojitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24,2025 wakati Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akifikishwa mahakamani hapo, likisisitiza atakayejitokeza atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Katazo la Jeshi la Polisi kwa wananchi ni kufuatia wito wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema,  John Heche kuwataka  wanachama wa chama hicho na wananchi kufika kwa wingi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24,2025 wakati Mwenyekiti wao Lissu  akifikishwa mahakamani kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili.

Heche ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika  viwanja vya Mbezi, wilaya ya Ubungo  Aprili 16,2025 wakati akihutubia mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza,  akiwahimiza wananchi hao kufika mahakamani hapo bila kuwa na silaha yeyote wala kufanya fujo bali wabebe vitambaa vyeupe na maji.

Akizungumzia wito huo, leo  Aprili 17,2025 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jeshi hilo limefuatilia mipango ya viongozi wa chama hicho na kubaini siku hiyo kutafanyika vurugu.

Muliro amesema lengo la vurugu hizo ni   kushinikiza mamlaka za kisheria kumwachia kiongozi wao ambaye anatuhumiwa.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawakumbusha wahusika kuwa Mahakama ni mamlaka za kisheria zilizo huru na hazipaswi kutishwa au kuingiliwa

wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

“Polisi  linawatahadharisha watu wote wanaohamasisha kuhusiana na nia hiyo ovu kutoshiriki kwenye mpango huo na linatoa onyo kali kuwa wale wote na wanaopanga ambao watajaribu kutekeleza kinachohamasishwa watashughulikiwa vikali kwa mujibu wa sheria za nchi,”amesema.

Lissu  alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza  na kusomewa shitaka la uhaini baada ya kukamatwa mkoani Ruvuma, alikokuwa kwenye ziara ya kuhamasisha ajenda ya chama hicho ya Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.

Kabla ya kusomewa shitaka hilo, taarifa ya Jeshi la Polisi iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco Chilya, ilieleza kuwa Lissu alikamatwa baada ya kuwepo madai ya kufanya uchochezi na hivyo jeshi hilo linamshikilia kwa mahojiano.

Katika hatua nyingine Kamanda Muliro amesema jeshi hilo  limejipanga  kuhakikisha waumini wa dini ya Kikristo wanasherekea siku hiyo kwa amani na utulivu.

“Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuwa na uangalizi wa karibu kwa watoto wakati wa matembezi na mikusanyiko mbalimbali, pia nyumba na makazi yasiachwe bila uangalizi wakati wa sherehe hizi.

Suala la usalama barabarani, tunasisitiza madereva wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria ili kuepusha ajali,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *