
Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini miradi saba ilikuwa na malimbikizo ya fidia zinazodaiwa jumla ya Sh24.75 bilioni, ikihusisha waathirika wa miradi 1,879.
CAG amebainisha hayo kwenye ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2023/24 baada ya kufanya mapitio kwenye miradi 360 ya maendeleo ikionyesha kutokamilishwa kwa malipo ya fidia hizo.
Kifungu cha 3(1) (g) cha Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 kinaelekeza watu, ambao haki zao za umiliki wa ardhi zimesitishwa au kumilikiwa na serikali kulipwa kwa fidia kamili, ya haki, na kwa wakati.
Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Utwaaji Ardhi, Sura ya 118 pia kinataka malipo ya fidia, pamoja na riba ya asilimia sita kwa mwaka kuanzia tarehe ya kumiliki ardhi hadi tarehe ya malipo, endapo ardhi itachukuliwa kabla ya malipo ya fidia kufanyika.
Katika ripoti yake, CAG amebainisha kwamba changamoto imebaki bila kutatuliwa huku baadhi ya miradi ikiwa imetekelezwa na mingine ikiwa katika hatua za kukamilika.
Miradi iliyobainishwa kwenye ripoti hiyo ni pamoja na Mradi wa Maendeleo ya Bonde la Msimbazi (MBDP) unaotekelezwa na Ofisi ya Rais, Tamisemi, wenye waathirika 1,034 wanaodai Sh10.9 bilioni huku hali ya utekelezaji ikiwa inaendelea.
Mradi mwingine ni ule wa Kusafirisha Umeme Mkubwa na Uwekaji Umeme Vijijini – Geita- Nyakanazi kilovoti 220 unaotekelezwa na Shirika la Umeme (Tanesco), ukiwa na waathirika 392, huku kiasi kinachodaiwa kikiwa ni Sh1.35 bilioni na utekelezaji ukiwa umefikia asilimia 99.
Miradi mingine na fedha zinazodaiwa ni Mradi wa Kuunganisha Umeme Kenya na Tanzania (Sh12.21 bilioni), Mradi wa Kufua Umeme katika Mto Malagarasi (Sh4.88 milioni), Mradi wa Usafirishaji wa Umeme Kigoma – Nyakanazi KV 400 (Sh176.6 milioni).
Pia, Mradi Endelevu wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha (Sh45.23 milioni) ambao umekamilika kwa asilimia 100 na Mradi Wa Umeme Wa Maji Wa Maporomoko ya Rusumo (Sh51.6 milioni).
“Ucheleweshaji wa fidia ulisababishwa na migogoro juu ya viwango vya fidia, kutokuwapo kwa baadhi ya watu walioathiriwa na miradi, nyaraka zisizokamilika na masuala ya uhamiaji yasiyotatuliwa.
CAG amebainisha kwamba changamoto hizo zinaathiri uhusiano na jamii. Pia, zinaweza kuhatarisha maendeleo endelevu ya miradi kwa siku zijazo, pamoja na kuongeza gharama ya fidia kutokana na mabadiliko ya kiuchumi.
“Ninapendekeza watekelezaji wa miradi waweke kipaumbele na kuharakisha mchakato wa malipo kwa watu walioathiriwa na miradi, washirikiane na mamlaka za serikali za mitaa na ofisi za usajili wa ardhi ili kuthibitisha umiliki wa ardhi na kutatua migogoro, ili kuhakikisha kuwa malipo yanafanywa kwa wakati,” anaeleza CAG katika ripoti hiyo.
Ucheleweshaji wa fedha
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha kwamba watekelezaji 17 wa miradi walichelewa kupata fedha za kutekeleza miradi, takribani Sh427.36 bilioni. Amesema ucheleweshaji huo ulitokana na michakato ya ndani ya muda mrefu na masuala ya mfumo wa malipo wa “D-Fund”.
Amebainisha kuwa utoaji wa fedha za miradi unatarajiwa kuendana na mzunguko wa bajeti na ratiba ya utekelezaji wa shughuli za miradi kama inavyoidhinishwa katika mpango kazi wa mwaka kwa kila mradi.
CAG amesema miradi 16 ilichelewa kupata fedha kwa kipindi cha hadi mwaka mmoja na Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ulichelewa kwa muda wa miaka hadi minne.
“Kuchelewa kutolewa kwa fedha kunaathiri utekelezaji kwa wakati wa shughuli za miradi. Ninapendekeza watekelezaji wa miradi wapunguze visababishi vya kuchelewa kupata fedha za miradi.
“Hatua hii itasaidia fedha za bajeti kupokelewa ndani ya muda uliokusudiwa ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa miradi na kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amebainisha CAG katika ripoti yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo.