RIPOTI YA CAG: Utitiri, mianya mifumo ya mapato kikwazo serikalini

Arusha. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam inatumia mfumo wa Tausi na N-Card kwa wakati mmoja kusimamia makusanyo ya viingilio katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli.

Mbali na stendi hiyo, pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) nazo zilitumia mifumo miwili.

Aidha, CAG amebaini udhaifu wa udhibiti wa ndani hususan katika mgawanyo wa majukumu kwenye mifumo ya Tehama ya uhasibu hali inayoongeza hatari ya udanganyifu na usimamizi mbaya wa fedha.

Stendi ya Magufuli ilizinduliwa Februari 24, 2021 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli ambapo aliagiza wasimamizi wa kituo hicho kukiendesha kwa kisasa.

Ujenzi wa kituo hicho kilichopo Mbezi ulianza Januari 11, 2019 na kukamilika Novemba 30, 2020 ambao uligharimu Sh50.9 bilioni zilizotolewa na Serikali Kuu.

Katika ripoti ya CAG ya Ukaguzi wa Mifumo ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa mwaka 2023/24 iliyowasilishwa bungeni jana Jumatano, Aprili 16, 2025 imeonesha kasoro hizo za kimfumo.

Ripoti hiyo imesema utumiaji wa mifumo miwili yenye matumizi yanayofanana unaongeza gharama za matengenezo na kuzuia lengo la Taifa la kuanzisha mfumo mmoja wa Serikali.

Amesema kifungu cha 25(1) cha Sheria ya Serikali mtandao ya mwaka 2019 kinaagiza kuandaliwa kwa mifumo endelevu wa kidijitali na ya kuaminika, ambapo  ukaguzi ulibaini kuwapo kwa matukio kadhaa ambapo kanuni hazikuzingatiwa kikamilifu.

CAG amesema Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inatumia mfumo wa ukusanyaji mapato ya Mamlaka za Serikali za za Mitaa (LGRCIS) kwa ajili ya kuandaa ankara mpya licha ya mfumo wa Tausi kuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

“Na kwa wakati mmoja kuendesha Mfumo wa Umma wa Huduma ya Maegesho ya Magari (TeRMIS) na Moduli ya Huduma za Maegesho ya Magari ndani ya Mfumo wa Tausi,” amesema CAG Kichere.

Ripoti imetaja Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga, inatumia mfumo wa usimamizi wa mapato ya kielektroniki ya Serikali na mfumo wa Vision Application kwa zaidi ya mwaka mmoja kusimamia michakato yake ya shughuli za taasisi.

“Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), linategemea mfumo wa Sage Pastel na AD-Software kusimamia orodha ya mali,” amesema.

Katika ripoti hiyo, CAG amesema:“Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hadi wakati wa ukaguzi wangu, lilikuwa linatumia mifumo miwili ya SDM na Nikonekt kusimamia maunganisho mapya ya umeme, licha ya kuwepo mipango ya kuhamia kwenye mfumo mmoja.”

Kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hadi wakati wa ukaguzi huo ilikuwa inatumia mifumo miwili kwa ajili ya uhamishaji fedha ambayo ni mfumo wa ndani wa uhamishaji na ukusanyaji fedha (FTCS) na SWIFT Alliance inayotolewa na mtoa huduma.

“Ninapendekeza menejimenti za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Tamisemi, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Tanga, ATCL, TRA na Tanesco zifanye tathmini na kuboresha mifumo yao ili kuondoa kujirudia na kuboresha michakato iliyopo,” amesema CAG Kichere.

Serikali imekuwa ikihimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika makusanyo ili kusaidia kuongeza mapato, kuepusha vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Aprili 2023, ukusanyaji wa mapato kwa mwezi mmoja katika stendi hiyo ulitajwa kuongezeka kutoka Sh3 milioni kwa siku hadi kufikia Sh5.7 milioni baada ya Manispaa ya Ubungo kuanza matumizi ya N-Card Februari 20, mwaka huo kwa lengo la kudhibiti upotevu wa mapato.

Mfumo huo mpya wa N-Card ulikuwa ukilalamikiwa kuchelewesha abiria huku baadhi ya madereva nao wakilalamikia ucheleweshaji wa safari zao.

Hatua ya matumizi ya mfumo huo yalilenga kupunguza foleni hasa wakati wa asubuhi, ambapo kunakuwa na abiria wengi na wasindikizaji wengi katika eneo hilo, pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato ambapo baadhi ya abiria walilalamikia baadhi ya milango kuchelewa kufunguka na kusababisha foleni.

Udhibiti wa bajeti katika mifumo

Aidha, CAG amebaini udhaifu wa udhibiti wa ndani hususan katika mgawanyo wa majukumu kwenye mifumo ya Tehama ya uhasibu hali inayoongeza hatari ya udanganyifu na usimamizi mbaya wa fedha.

Amesema taasisi nyingi ziliruhusu watumiaji kuanzisha na kuidhinisha miamala katika mifumo ya uhasibu pamoja na udhibiti wa bajeti ambapo mifumo iliruhusu matumizi kuzidi viwango vilivyoidhinishwa.

CAG ametoa mifano ya udhaifu wa mgawanyo wa majukumu katika mifumo ya uhasibu wa Serikali ikiwemo Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE), ambapo katika baadhi ya taasisi mtumiaji mmoja alikuwa na uwezo wa kuanzisha na kuidhinisha mgao wa fedha.

“Uhamishaji wa fedha, usimamizi wa akaunti za wazabuni na urejeshaji wa posho za safari na pia akaunti ya ‘system’ ilitumiwa kuunda, kuidhinisha, na kutuma marekebisho ya hesabu za mwisho,” amesema.

Kuhusu mfumo wa Usimamizi wa Rasilimali (ERMS), unaotumiwa na Bodi ya Nafaka Mchanganyiko na Mamlaka ya Serikali Mtandao amesema mhasibu mmoja alikuwa na mamlaka ya kuhamisha fedha, kuidhinisha mgao wa fedha na kutoa posho za safari bila udhibiti huru.

Amesema kwenye mfumo wa Epicor, unaotumiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji, mtumiaji mmoja aliweza kuunda na kuidhinisha mikataba midogo ya ununuzi wa ndani na hati za kupokelea mali bila ukaguzi wa mtu mwingine.

“Mwenendo huu ulionekana pia kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambapo mtumiaji mmoja alikuwa na mamlaka ya kuanzisha na kuidhinisha ankara na vocha za malipo,” amesema CAG Kichere.

CAG amesema katika mfumo wa Jeeva, unaotumiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kwenye  mfumo huo mtumiaji mmoja alikuwa na mamlaka ya kuunda, kuidhinisha na kutuma vocha za malipo na marekebisho ya hesabu.

“Ninapendekeza menejimenti za taasisi husika ziboreshe mifumo ya kifedha kwa kuweka na kutekeleza udhibiti madhubuti wa bajeti na uidhinishaji huru ili kuhakikisha matumizi hayazidi viwango stahiki,” amesema CAG Kichere.

Muse yashindwa kusimamia madeni

Kuhusu matumizi ya mifumo mingi ya uhasibu, CAG amesema hali hiyo inaweza kusababisha kutokuwa na ufanisi, utofauti wa taarifa, gharama kubwa za uendeshaji na changamoto katika upatanisho wa data na utoaji wa taarifa za kifedha.

Amesema ilibainika Mfumo wa Uhasibu Serikalini (Muse) ulikuwa na upungufu mkubwa katika kuweka kumbukumbu za madeni hali iliyosababisha taasisi kulazimika kutumia mifumo mingine ya uhasibu ili kusimamia miamala ya fedha kwa ufanisi.

Ametolea mfano Chuo Kikuu cha Mzumbe, kiliendelea kutumia mfumo wa Sage 300 sambamba na Muse kwa ajili ya usimamizi wa madeni ya miaka ya nyuma kutokana na mapungufu ya Muse.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linatumia mfumo wa Navision ambao uliunganishwa na Mfumo wa Taarifa wa Usimamizi na Upimaji wa Ubora, kusimamia madeni ya miaka ya nyuma kutokana na Muse kushindwa kushughulikia ipasavyo.

“Bodi ya Pamba Tanzania ilitumia mfumo wa Sage Pastel kutunza kumbukumbu za madeni yanayohusiana na wauzaji, wakati wa malipo yalishughulikiwa kupitia Muse, hali iliyosababisha gharama za matengenezo na msaada wa kiufundi kwa mfumo huo wa Sage Pastel,” amesema na kuongeza:

“Ninapendekeza menejimenti ya Wizara ya Fedha iboreshe Muse ili uweze kusimamia kwa ufanisi zaidi madeni, kuboresha utendaji wa mifumo ya kifedha, kupunguza gharama na kuongeza usahihi wa data na uaminifu wa taarifa za kifedha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *