Huyu ndiye Nawa, mwigizaji wa Isidingo aliyefariki Afrika Kusini

Dar es Salaam. Moja ya taarifa zilizowashitua wengi ni kuhusu kifo cha mwigizaji wa Isidingo, Don Nawa aliyefariki dunia Aprili 16, 2025. Mfahamu zaidi.

Jina lake halisi ni Don Mlangeni Eric Nawa, alizaliwa Juni 7, 1959 huko Boksburg, Transvaal, Afrika Kusini. Alijulikana zaidi kwa uhusika wake kama Zebedee “Bra Zeb” Matabane katika tamthilia ya muda mrefu ya Isidingo.

Safari yake ya uigizaji ilianza katika majukwaa ya michezo ya kuigiza kabla ya kuhamishia nguvu kwenye televisheni. Ambapo mwaka 1989 alipata nafasi ya kwanza ya uigizaji wa televisheni kama David kupitia Tamthilia ya ‘Zulu Ubambo Lwami’.

Baada ya safari yake kuanzia hapo, jamii ilianza kumtambua zaidi mwaka 1992 kupitia uhusika wa Zakhe katika tamthilia ‘Hlala Kwabafileyo’ pamoja na tamthilia ya vichekesho ya ‘Sgudi Snaysi’ iliyotoka mwaka 1993.

Lakini alikuja kujipata kupitia uhusiaka wake kama Zebedee Matabane katika Tamthilia ya Isidingo, ambapo aliigiza kuanzia mwaka 1998 hadi 2014. Huku kuondoka kwake kukihusishwa na mgogoro na Kampuni ya Endemol South Africa pamoja na mtayarishaji wa Tamthilia ya Isidingo.

Baada ya kutemana na Isidingo, aliendelea kuonesha ukubwa wake katika uigizaji akionekana kwenye tamthilia kama The Throne (2018–2019), The River (2018, 2023), The Estate (2021–2023), na Shaka iLembe (2023). Pia alionekana katika filamu Losing Lerato mwaka 2019 kama Kamanda wa SWAT.

Tuzo alizonyakua 
Katika miaka yake ya uigizaji Dom amewahi kunyakua tuzo mbalimbali ikiwemo ya Golden Horn ya SAFTA kama Mwigizaji Bora katika thamthilia ya Televisheni mwaka 2006, vilevile mwaka 2018, alitunukiwa Tuzo ya Lifetime Achievement katika ‘Royalty Soapie Awards’ kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya televisheni ya Afrika Kusini.

Mchango wake kwenye tasnia ya filamu Afrika Kusini 
Don Nawa alikuwa moja ya nguzo muhimu katika tasnia ya filamu na televisheni ya Afrika Kusini kwa zaidi ya miongo mitatu. Mchango wake katika tasnia ya uigizaji iligusa nyanja mbalimbali huku akileta mabadiliko chanya katika uhusika wake. Lakini pia kufundisha na kuwaelekeza waigizaji chipukizi ambao wanafanya vizuri.

Nawa anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola za Kimarekani 150,000 hadi 200,000 sawa na Sh 400 milioni hadi 540. Utajiri huo aliupata katika kusaini mikataba ya Tamthilia ikiwemo Isidingo, ‘Sgudi ‘Snaysi, The Estate nk.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *