
Moshi. Mashirika ya Umma yapatayo 106, ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), yanadai madeni ya biashara yanayofikia Sh3.58 trilioni ambazo ni madeni ya huduma walizotoa kwa wateja hadi kufikia Juni 30, 2024.
Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyokabidhiwa bungeni jana Jumatano, Aprili 16, 2025 inaeleza madai ya biashara yaliendelea kuathiri mtiririko wa fedha wa mashirika na uwezo wao wa kutekeleza shughuli zilizopangwa.
Katika taarifa hiyo CAG amebainisha NHIF inadai Sh180 bilioni kama mikopo kwa mashirika manne ya Serikali, huku Sh28 bilioni za riba zikiwa zimekwishatolewa kama hasara katika mwaka uliopita.
“Hakukuwa na marejesho yoyote katika mwaka husika kinyume na mikataba ya mkopo. Hii inatokana na ucheleweshaji wa Serikali katika kusimamia na kulipa madeni yake ya ndani. Hali hii inahatarisha uwezo wa mfuko,” ameeleza CAG.
Mbali na NHIF, hali ni kama hiyo katika Bohari ya Dawa (MSD) ambapo hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024, CAG alibaini bohari hiyo ilikuwa na madai ya Sh267.79 bilioni ukilinganisha na deni la mwaka uliopita la Sh280.93 bilioni.
“Deni hili linahusiana na gharama za Bohari ya Dawa katika upokeaji, uhifadhi, na usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu vilivyotolewa kama msaada,” amesema.
“Madai haya makubwa yanaathiri mtaji wa MSD, uwezo wake wa kuwa na kiwango sahihi cha bidhaa, na shughuli zake. Serikali inapaswa kulipa deni hili ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa bajeti na kupunguza changamoto za kifedha,” amesema.
Bodi ya mikopo na NHC
Katika ukaguzi huo, CAG amebaini deni linalohusu urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika limeongezeka kwa Sh123.04 bilioni hadi kufikia Sh931.14, ongezeko la asilimia 15 kutoka mwaka uliopita uliokuwa na deni la Sh808.11 bilioni.
“Ucheleweshaji wa marejesho haya unatokana na ukosefu wa ufuatiliaji wa kutosha wa wadaiwa,” alisisitiza CAG katika taarifa yake hiyo.
Kwa upande wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), CAG alibaini kuwa wapangaji 3,440 waliokuwa na madeni ya Sh19.09 bilioni kwenye mfumo wa bili kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, walihama bila kulipa madeni yao.
“Uongozi wa Shirika ulieleza kuwa wadaiwa hawa bado wanafuatiliwa na wakusanya madeni. Tatizo hili linatokana na udhibiti hafifu wa mfumo wa ankara na ukusanyaji wa mapato, hali inayohatarisha hasara ya kifedha kwani kuna uwezekano mkubwa wa madeni haya kutolipwa kabisa,”alieleza CAG.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
CAG anasema kwa mujibu wa Sera ya Mkopo ya mwaka 2014, hospitali haipaswi kutoa huduma kwa mkopo kwa taasisi zenye historia ya kutolipa madeni yao.
Sera hiyo kinataka huduma kusitishwa kwa wateja wenye madeni yaliyozidi siku 60 tangu kutolewa kwa ankara lakini hospitali hiyo ilikiuka sera hiyo kwa kutoa huduma za Sh4.28 bilioni kwa taasisi zilizo na madeni ya Sh6.71 bilioni.
Mbali na taasisi hizo, lakini ilitoa mikopo ya Sh16.6 bilioni kwa wagonjwa binafsi.
“Madeni ya Sh3.08 bilioni yaliyopitiliza muda hayakuwasilishwa kwa wakusanya madeni kama inavyotakiwa na sera”alisema CAG katika taarifa yake.
“Haya yote yanatokana na udhaifu katika ukusanyaji wa madeni, utekelezaji hafifu wa sera, na changamoto za mfumo wa usimamizi wa madeni. Hali inayosababisha matatizo ya kifedha na kuathiri utoaji wa huduma bora za afya”
Madai yasiyo hai
Katika ukaguzi huo, CAG amebaini mashirika ya umma ikiwemo MSD, TTCL na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili zinakabiliwa na changamoto kubwa za usimamizi wa madai.
Lakini pia madai ya muda mrefu yanaendelea kutokusanywa kwa miaka kadhaa, alisema CAG katika ukaguzi huo unaoishi Juni 30, 2024.
“Bohari ya Dawa ina akaunti za wateja wasio hai na madeni yasiyolipwa ya Sh7.93 bilioni, wakati, Shirika la Mawasiliano Tanzania lina wateja wa muda mrefu wasiofanya biashara na shirika wenye madeni ya Sh27.19 bilioni,” amesema.
“Pia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kimekabiliwa na changamoto ya madeni yasiyo hai ambayo hayajakusanywa kwa muda mrefu yenye thamani ya Sh90.67 milioni,” alisisitiza CAG.
Kwa mujibu wa CAG, changamoto hizo zinasababishwa na ukosefu wa maridhiano ya hesabu, udhaifu wa hatua za utekelezaji wa ulipaji, na kumbukumbu za wateja zisizo sahihi, jambo linaloathiri mtiririko wa fedha na uendelevu wa shirika husika.
CAG amependekeza mashirika husika ya umma yaboreshe mifumo ya udhibiti wa ndani katika ukusanyaji wa madeni, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wadaiwa wote ili kuhakikisha kuwa wanamaliza madeni yao.
Mashirika 36 yanajiendesha bila bodi
Katika ripoti hiyo, CAG amesema kuna mashirika ya umma yasiyokuwa na bodi za wakurugenzi, imeongezeka kwa asilimia 350 hadi kufikia mashirika 36.
“Niligundua idadi ya mashirika ambayo hayakuwa na bodi ya wakurugenzi hadi kufikia Februari 2025 iliongezeka na kufika 36 ambapo yamekosa bodi hizo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi 24,” alisema.
Hata hivyo, CAG alisema amebaini Serikali ilichukua hatua na kuteua bodi ya wakurugenzi katika mashirika ya umma saba kati ya mashirika manane ambayo hayakuwa na bodi ya Wakurugenzi kama ilivyoripotiwa mwaka 2022/2023.
Kwa mujibu wa CAG, Serikali haikufanya uteuzi katika bodi ya Pareto Tanzania.
Idadi ya mashirika ambayo hayakuwa na bodi ilipungua kwa asilimia 38 kutoka mashirika 13 mwaka 2021/2022 hadi mashirika manane mwaka 2022/2023, hali iliyoonesha kuimarika kwa mchakato wa teuzi za bodi za wakurugenzi.
Kulingana na CAG, katika mwaka 2023/24, idadi ya mashirika yasiyokuwa na bodi za wakurugenzi iliongezeka hadi kufikia 36, ikionesha kuzorota kwa juhudi za awali za michakato ya teuzi za bodi za wakurugenzi.
CAG amependekeza mashirika ya umma kufanya kazi kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha teuzi za wajumbe wa bodi zinafanyika kwa wakati mara tu mjumbe wa bodi atakapopangiwa majukumu mapya serikalini.
Pia ameitaka Ofisi ya Msajili wa Hazina iweke mfumo wa kufuatilia muda wa uanachama wa wajumbe wa bodi na ichukue hatua za kuanza mchakato wa teuzi miezi sita kabla ya muda wa uanachama wa wajumbe wa bodi kumalizika.
CAG alibaini mashirika ya umma 12 yalipata changamoto katika kutekeleza majukumu yake, kama vile kukosekana kwa kamati za bodi, mkataba wa bodi na makubaliano ya mikataba ya utendaji katika bodi hizo za wakurugenzi.
Hii ilisababisha changamoto kubwa katika uwajibikaji katika mashirika ya umma na tatizo hilo lilitokana na ukosefu wa ufahamu katika mashirika ya umma kuhusu hitaji la kusaini mikataba ya utendaji baina yake na Ofisi ya Msajili wa Hazina, kuundwa kwa kamati ya bodi pamoja kuwa na mikataba ya bodi.
CAG katika ripoti yake alisema kukosekana kwa miongozo ya Serikali, kunaathiri ufanisi wa mashirika, Serikali kushindwa kutimiza malengo yake, kuongezeka kwa vihatarishi, kuzorota kwa ukwasi, na kupoteza imani ya wadau.
Amependekeza bodi za wakurugenzi za mashirika ya umma kuhakikisha nyenzo na miongozo ya Serikali zipo, kama vile mikataba ya bodi, kuunda kamati za bodi na pia kuhakikisha mikataba ya utendaji na uwajibikaji imesainiwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, CAG amebaini Mamlaka ya Usimamizi wa Bima haikuwa imeanzisha idara na mfumo wa kusimamia bima ya afya kwa wote, kinyume na kifungu cha 7 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na.13 ya mwaka 2023.
Pia alibaini Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita haikuwa imeanzisha Kitengo cha huduma za kisheria, Kitengo cha Tehama pamoja na Kitengo cha Takwimu ambavyo vilitakiwa kuwepo kulingana na muundo wa mashirika.
Hali hiyo ilisababishwa na kasi ndogo katika utekelezaji wa maazimio ya kuanzisha kurugenzi pamoja na mfumo wa kusimamia Bima ya Afya kwa Wote.
Halikadhalika CAG alibaini kuwepo kwa ucheleweshaji wa kutoa ajira katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita hali inayoleta changamoto katika kutekeleza muundo.
Kushindwa kutekeleza kwa ukamilifu miundo, na mifumo iliyoidhinishwa kunadhoofisha usimamizi wa udhibiti, kuchelewesha utoaji wa huduma, na inaweza kusababisha kupungua kwa ufanisi.
CAG amependekeza mashirika ya umma yahakikishe miundo na mifumo ya mashirika iliyoidhinishwa na mamlaka husika inatekelezwa kikamilifu na mashirika yote yahakikishe yanaajiri watumishi wenye sifa, ili kujaza idara na vitengo vyote vilivyo wazi.