
Dar es Salaam. Wakati vyama vya siasa vikiendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amebainisha mambo matatu yanayopaswa kuzingatiwa ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na kupata wawakilishi sahihi wa wananchi.
Jaji Warioba amesema hayo katika mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) yaliyofanyika Jumanne, Aprili 15, 2025 ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.
Jambo lingine, amesema ni kuhakikisha sera na lugha zinazotumika na wanasiasa zinaimarisha mshikamano, umoja na amani badala ya kuuvunja.
Mchakato wa uteuzi, rushwa
Katika ufafanuzi wake kuhusu hayo, Jaji Warioba amesema ili kupatikana viongozi wanaowawakilisha wananchi, ni muhimu mchakato wa uteuzi wao uzingatie kukubalika kwao.
Katika kulifanikisha hilo, amesema hapana budi kudhibiti mianya ya rushwa katika michakato ya uteuzi wa wagombea ndani ya vyama vya siasa.
“Kwa kipindi hiki, umekuwa ushauri wetu kwamba vyama vya siasa vingechukua hatua zinazozuia rushwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea,” amesema.
Kwa bahati nzuri, amesema katika siku za karibuni amekutana na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Tundu Lissu pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kwa nyakati tofauti, na wote wameonyesha wanavyofanya juhudi za kudhibiti rushwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Lissu alimweleza walivyopambana kudhibiti rushwa wakati wa uchaguzi wao wa ndani na Dk Nchimbi alimweleza namna walivyopanua wigo wa wajumbe wanaopiga kura za maoni kuwateua wagombea ili kuzuia rushwa.
Amesema hiyo ni hatua nzuri kwa vyama hivyo, lakini muhimu ni kuhakikisha usimamizi unakuwa wa dhati kiasi cha kutoruhusu rushwa.
Amelieleza hilo, akirejea historia ya chama cha Tanganyika African National Union (Tanu), iliyoweka utaratibu wa kuipa kamati kuu mamlaka ya kuteua wagombea bila kupata maoni ya wananchi wa ngazi za chini.
Amesema hilo lilikoma pale alipotokea mwanachama aliyeteuliwa na kukataa akidai anagombea kama mgombea binafsi.
Amesema hatua ya mwanachama huyo, iliisababisha Tanu ibadili utaratibu kutoka uongozi wa juu kuteua wagombea hadi mchakato huo kuhusisha wananchi wa chini.
Baadaye ulipoanza mfumo wa siasa za chama kimoja, amesema Tanu ilikuwa ikipeleka wagombea wawili majimboni ili achaguliwe mmoja. Kati ya wawili hao, amesema chama hicho kilisababisha mgombea mmoja mwenye nguvu anamshinda mwenzake.
Amesema ulifika wakati wananchi walimpa kura yule aliyeonekana dhaifu na mara kadhaa walishinda, huku wale waliotakiwa na chama wakishindwa pamoja na umaarufu wao.
“Ndiyo ikaanzishwa sasa tuwe tunateua baada ya kupata maoni ya wananchi, tukaanza sasa kura za maoni,” amesema Jaji Warioba aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Amesema baadaye rushwa ikaonekana kuingia kwenye mchakato na uamuzi ulifanywa kuongeza wajumbe wanaopiga kura.
Hiyo haikutosha, amesema bado rushwa iliendelea na hata waliporuhusu wanachama wote bado ilikuwepo.
“Kwa hiyo rushwa lazima itakuwepo, hata katika taratibu hizi walizoweka, utakuta hata walioweka kuchuja nao wanahongwa. Katika kufanya mchujo lazima wawe na uhakika kwamba rushwa haijaingia,” amesema.
Amesema hata watatu watakaochaguliwa ni muhimu kuhakikisha nafasi za kutoa rushwa zinadhibitiwa.
“Nimevutiwa na hatua zinazochukuliwa kudhibiti rushwa, lakini bado na tutaona mwaka huu, pamoja na hatua hizi kama rushwa itadhibitiwa,” amesema.
Amesema katika mchakato wa uteuzi wa wagombea, maoni ya wananchi ni jambo muhimu kwa sababu ndiyo yanayoamua kupatikana mgombea anayekubalika.
Lissu, Nchimbi
Februari 10, 2025, Lissu akiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa walimtembelea Jaji Warioba ofisini kwake, Dar es Salaam.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Chadema ilieleza, Lissu alifanya mazungumzo na Jaji Warioba kuhusiana na masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi wa ndani wa chama hicho. Pia, walizungumzia hali halisi kuhusiana na uchaguzi uliomalizika wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji wa Novemba 27, 2024 na ulazima wa kuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi Tanzania ili kuwa na chaguzi zinazoaminika na zisizo na dosari.
Februari 20, 2025, Dk Nchimbi alimtembelea Jaji Warioba nyumbani kwake Dar es Salaam. Taarifa kwa umma iliyotolewa na CCM ilieleza Jaji Warioba alipongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na chama hicho katika mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi.
Taarifa hiyo ilimnukuu Jaji Warioba akisema vita dhidi ya rushwa si ya siku moja, CCM haina budi kuhakikisha mapambano ya kumshinda adui huyo yanakuwa endelevu kwa kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.
Aidha, Jaji Warioba, mbali na kukumbusha kuhusu misingi ya CCM, alisisitiza sifa na miiko ya uongozi ilivyoainishwa kwenye Katiba ya CCM, akisema chama kina wajibu wa kuendelea kuwapatia matumaini Watanzania kwa kutoa uongozi bora kwa mwelekeo sahihi wa nchi.
“Vita hii si ya siku moja, ni muhimu muda wote chama kitafute njia za kuzuia rushwa kwa kusimamia misingi yake. Watu wazungumzie sifa na miiko ya uongozi. Wazungumzie sera, si hela. Kihistoria, CCM ni chama cha itikadi, sera na ilani. Kina wajibu wa kuonesha matumaini wapi tunawapeleka watu,” alisema Jaji Warioba.
Dosari za kisheria
Akifafanua jambo la pili la kufanikisha uchaguzi wa amani, Jaji Warioba amesema kuhakikisha sheria, kanuni na Katiba zinawezesha wananchi kushiriki mchakato huo.
“Kuna sheria zinazotungwa kuwawezesha watu wakapige kura na kuna sheria zinazotungwa kuwadhibiti watu wasipige kura,” amesema Jaji Warioba.
Ametolea mfano mwaka 1958, akisema wakoloni waliweka sheria na masharti magumu ya kupiga kura, ikiwemo kigezo cha kuwa msomi wa kidato cha nne, kilichokuwa kigumu kwa wakati huo.
Amesema kwa vigezo hivyo, wapigakura walikuwa wachache, chini ya 50,000 licha ya idadi ya watu wakati huo kuwa zaidi ya milioni tisa.
Baada ya uhuru, amesema mabadiliko yalifanyika kuhakikisha watu wanawezeshwa kushiriki uchaguzi.
Amesema isivyo bahati hivi sasa watu wanaenguliwa nje ya misingi iliyowekwa katika Katiba, badala yake inafanyika kwa kufuatwa kanuni.
Jaji Warioba amesema Katiba haikueleza makosa ya kuandika majina kama kigezo cha mgombea kuenguliwa.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti mamlaka zinazohusika na uchaguzi ikiwemo INEC na Tamisemi zimekuwa zikitolea ufafanuzi kuhusu dosari zinazosababisha wagombea wa vyama mbalimbali vya siasa kuenguliwa ama kuwekewa mapingamizi na wagombea wengine.
Sera, lugha
Katika mahojiano hayo, Waziri Mkuu huyo mstaafu amesema ili kuwa na uchaguzi wa amani ni muhimu kuepuka lugha na sera zinazodhoofisha umoja, mshikamano na amani.
Amesema katika uchaguzi lazima kujitahidi kuhusu sera, lugha zinazodumisha Muungano ambao ni gundi ya umoja, mshikamano na amani.
Hoja yake hiyo, inatokana na kile alichoeleza kuwa ameshuhudia siku za karibuni watu wakitoa lugha zinazovunja umoja, zinahamasisha ukabila, udini na ukanda.
“Unaona sasa kunaanza kuwa na ubaguzi wa kanda, lakini zaidi unaanza kuzuka utaifa, utaifa wa Tanganyika, utaifa wa Zanzibar,” amesema.
Amesema amesikia maneno mara kadhaa watu wakisema mtu fulani hawezi kuchaguliwa kwa sababu ni Mzanzibari, ama huyu hawezi kwa sababu ni Mtanganyika.
“Hii ni hatari, tukianza kubaguana wananchi wa Bara na Zanzibar,” amesema.
“Kama Wazanzibari si wafanyaji kazi wazuri,” amesema, “mbona Mwalimu Nyerere alimteua Dk Salim Ahmed Salim kwa nafasi mbalimbali ikiwemo ya uwaziri mkuu na alitumikia Taifa kwa uadilifu na anasifika hadi sasa?”
Amesema hata mwaka 2005, Dk Salim alishawishiwa agombee urais na watu kutoka Bara na hata timu iliyozunguka kwenda kuomba kuungwa mkono ilihusisha Wabara zaidi na Mzanzibari mmoja.
Amesema kubaguana huko ni hatari kwa mustakabali wa umoja wa kitaifa.
“Ubaguzi wa aina hii utadhoofisha umoja wetu na amani yetu. Mwalimu alisema dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya binadamu. Ukishaila, hutaacha, utaendelea,” amesema akionesha kusikitishwa na kauli hizo na kutaka zikomeshwe.
Amewataka viongozi wote wa vyama vya siasa wajitahidi kuepuka mbinu zitakazoingilia amani ya nchi katika uchaguzi na nyakati zote.