Nairobi. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amson Group, Edha Nahdi, amekutana na Rais wa Kenya, William Ruto Ikulu jijini Nairobi kwa ajili ya mazungumzo kuhusu uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa kiwanda cha saruji cha Bamburi kwa awamu ya pili.
Uwekezaji huo una thamani ya Dola za Marekani milioni 380 (Zaidi ya Sh960 bilioni).
Nahdi (37) amenunua Kampuni ya Bamburi Cement kwa thamani ya Sh500 bilioni (Dola za Marekani milioni 182), hatua iliyoandika rekodi kuwa uwekezaji mkubwa zaidi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi.

“Amson Group imeonesha nia ya kuwekeza pia nchini Uganda, baada ya Bamburi Cement kukamilisha uuzaji wa hisa zake asilimia 70 katika kampuni tanzu ya Hima Cement kwa kampuni za Sarrai Group na Rwimi Holding, kwa thamani ya takribani Dola za Marekani milioni 84 (Sh214 bilioni) Machi 2024,”amesema Nahdi baada ya mazungumzo hayo
Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unatajwa kama uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kwa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Uwekezaji huu unaimarisha nafasi ya Amson Group kupanua shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Amson Group, inayomilikiwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, na sasa inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki.