
Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, imemuhukumu Naufali Ramadhani (22) na Abubakari Chiputa, kifungo cha nje cha miezi sita kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa chaja ya baiskeli na extension cable.
Pia, Mahakama hiyo imeamuru chaja hiyo pamoja na extension cable arudishiwe mlalamikaji, ambaye ni Idriss Mustafa.
Uamuzi huo umetolewa jana Jumatano Aprili 16, 2025 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Claudius Kipande, baada ya washtakiwa hao kukiri shitaka hilo, walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza kusomewa shitaka lao.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Karani wa mahakama hiyo, Emmy Mwansansu, aliwasomea shitaka lao.
Mwansansu alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo, Aprili 11, 2025 saa 4:00 asubuhi katika Mtaa wa Alkhani, Kata ya Upanga, wilaya ya Ilala.
Washtakiwa hao walitenda kosa la wizi kinyume na kifungu 258 na 265 Sura ya 16 ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Karani Mwansansu alisema washtakiwa hao siku ya tukio, waliiba chaja ya baiskeli na extension cable yenye thamani ya Sh120,000 mali ya Idriss Mustafa, huku wakijua kuwa kitendo hicho ni kosa na kinyume cha sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa baada ya kusomewa shitaka hilo, walikiri na ndipo hakimu alipowahukumu.
Hata hivyo, washtakiwa hao waliomba wapunguziwe adhabu kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza.
“Mahakama imewatia hatiani kama mlivyoshtakiwa baada ya kukiri shitaka lenu, hivyo inawahukumu kifungo cha nje cha miezi sita na mahakama inaamuru chaja pamoja na extension cable mliyoiba mumrudishie mlalamikaji,” alisema Hakimu. Na washtakiwa hao wamerudisha vifaa hivyo.