SAKATA KUZUIA MAZAO: Wadau waunga mkono, watoa tahadhari

Dar es Salaam.  Wakati Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ikitangaza itazuia mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini, wadau wameunga mkono hatua hiyo lakini wakitoa tahadhari kuwa ina athari za kiuchumi.

Waziri Bashe kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii leo Arpili 17, 2025 amesema ifikapo Jumatano Aprili 23, 2025 Serikali ya Tanzania itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka mataifa hayo.

Amesema Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwamo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi.

“Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi,” amesema.

Kuhusu Afrika Kusini amesema: “Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka 10 katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda masilahi ya nchi yetu.”

Amesema kutokana na hali hiyo na baada ya juhudi zote za kidiplomasia kufanyika bila mafanikio, iwapo Serikali za Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano Aprili 23, 2025 Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili.

“Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania kuelekea Bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote hadi zuio hilo litakapoondolewa,” amesema.

Bashe amesema usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda masilahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania.

“Wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo, ninawashauri kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapobadilisha msimamo wao,” amesema.

Waziri amesema wafanyabiashara walioweka oda za apples (tufaa), machungwa na bidhaa zingine ambazo hununuliwa Afrika Kusini, wanashauriwa kuacha kwa sasa kwani hawataruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapofungua soko la ndizi.

“Ninathibitisha kuwa, kama waziri mwenye dhamana nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi. Hatua hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu na usawa katika biashara za kikanda,” amesema.

Maoni ya wadau

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva (Tadwu), Schubert Mbakizao ameunga mkono hatua ya Serikali akisema lazima Tanzania ilinde heshima yake.

Ingawa magari yanapozunguka ndipo madereva na waajiri hupata kipato, lakini linapokuja suala kama hilo amesema hawajali kupata hasara.

Amesema hata tamko litakapotolewa na wakakaa mpakani, wako tayari lakini heshima ya nchi ilindwe.

“Kwa sasa magari mengi yanaingia na kutoka mpakani, endapo Serikali ikitangaza najua yapo yatakayobaki na athari zinapatikana pande zote mbili kwa madereva na waajiri wao.

“Nasema nakubalina na hili kwa sababu sisi Watanzania tunayowatendea wenzetu, wenyewe hawatutendei,” amesema.

 “Naunga mkono kulinda heshima ya Tanzania, haiwezekani wazuie bidhaa zetu halafu zao ziingie tu. Ni sahihi tuumie kwa ajili ya kujenga heshima hata wakisema tukae miezi miwili sisi tuko tayari.”

Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Donath Olomi amesema kwa jumla vita vya namna hiyo havisaidii bali vitaharibu pande zote kwa kuwa biashara zitaathirika.

Amesema inapaswa Serikali zote zikae mezani kujadili suluhisho la changamoto zilizopo, kuliko kuanza yaliyokusudiwa kwa kuwa athari zake zinagusa uchumi, ajira, wakulima na wafanyabiashara.

“Hata waziri husika hajasema tuzuie moja kwa moja ametoa muda ili kama ikiwezekana Serikali zote zikae mezani. Kama kuna kitu kirekebishwe basi ifanyike hivyo, biashara ziweze kuendelea,” amesema.

Amesema endapo ikitokea ugomvi watu wanatishiana ila kabla ya kuanza kupigana wanakuwa na namna ya kumaliza ugomvi huo, namna hiyo ni kuelewana ili kuepuka madhara.

“Vita vya kibishara ni vibaya, tunapeleka bidhaa zetu kwa kuwa kuna biashara, watu wao kadhalika. Hapa maana yake kuna soko la wakulima na wafanaybiashara,” amesema.

Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude amesema ni bahati mbaya kwa nchi za Afrika kufikia hatua hiyo akieleza kitendo cha namna hiyo kitaumiza pande zote husika.

Amesema hali hiyo itaumiza wakulima wanaopata changamoto kuanzia shambani, akihoji watapeleka wapi bidhaa zao.

“Tanzania na Afrika Kusini zina uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara. Kitendo hicho kitaumiza pande zote mbili kwa sababu soko litapotea na athari zake kiuchumi ni kubwa. Mnyororo mzima wa kibiashara utaathirika kwa kuwa wanaopeleka bidhaa huko watakosa soko na itaumiza kiuchumi,” amesema.

Amesema hali hiyo ikiendelea kwa muda mrefu itakuwa, mbaya zaidi kutokana na wahusika kupunguza uzalishaji na pia suluhisho kwao linaweza kuwa kutafuta soko jipya japokuwa si kazi rahisi.

Mkude amesema nafasi za kidiplomaisa zinapaswa kutumika ili kumaliza tofatuti zilizopo.

“Wakati huu tuna soko huru la Afrika ambalo linaunganisha bara zima kuuziana bidhaa sisi kwa sisi, sasa mambo kama haya hayatakiwi kuwapo,” amesema.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano amesema mara nyingi hadi Wizara kutaka kuchukua hatua kama hiyo inakuwa imeshafanya tathimini na kujiridhisha.

“Tanzania imeshajeruhiwa kwa muda mrefu kutokana na vikwazo vya kibiashara vya namna hiyo. Wenzetu wamekuwa kama wabinafsi na Serikali kuchukua hatua hii ni sahihi kwa sababu inajibu mapigo kama ilivyo China na Marekani,” amesema.

Amesema Tanzania inalinda watu wake, wakiwamo wakulima ingawa kuna matokeo hasi kama vile kupoteza soko la bidhaa kwa pande zote.

“Kuna bidhaa kama apples (tufaa) tunalima Njombe yanaweza yakatumika hapahapa kwani kuna namna tunajimudu na soko la ndani, ushauri wangu tunapaswa kukaa mezani,” amesema.

Kati ya Aprili na Mei, 2021 mahindi ya Tanzania yalizuiwa kuingia nchini Kenya kwa maelezo kwamba yana sumu kuvu.

Baadaye Taifa hilo liliwataka wafanyabiashara wanaoingiza mahindi kutoka Tanzania kuhakikisha wana cheti kinachoonyesha yamepimwa na kiwango cha sumu kuvu ni kile kinachokubalika kimataifa.

Hata hivyo, viongozi wakuu wa mataifa hayo walikutana kwa mazungumzo na baadaye biashara ilirejea katika hali ya kawaida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *