Musoma. Serikali mkoani Mara imejenga nyumba mpya tatu na kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba 33 za wakazi wa Manispaa ya Musoma, baada ya nyumba zao kuharibiwa na mvua zilizoambatana na upepo mkali usiku wa kuamkia Machi 23, 2025.
Taarifa hiyo imetolewa leo Alhamisi Aprili 17, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, wakati akipokea msaada kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa Mtambi, zaidi ya kaya 300 ziliathirika kwa kupoteza makazi yao baada ya nyumba zao kubomolewa na kuezuliwa mapaa, hivyo baadhi yao kuishi kwenye kambi za muda zilizowekwa na Serikali.
“Tulibaini kuwa nyumba tatu ziliharibika kabisa na wamiliki wake hawakuwa na uwezo wa kujenga upya, huku nyumba nyingine 33 zilihitaji ukarabati mkubwa. Serikali ilianzisha ujenzi wa nyumba hizo tatu kuanzia msingi na kukarabati nyingine kwenye sehemu za kuta na paa kwa lengo la kuwasaidia wananchi kurejea katika maisha yao ya kawaida au kuwa na makazi bora zaidi,” amesema Mtambi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi wote mkoani humo hasa wanaoishi maeneo hatarishi kama mabondeni, wahame ili kuepuka madhara zaidi kipindi hiki cha mvua.
“Nyumba nyingi ziliharibika kutokana na nguvu ya kimbunga. Tunawashauri wananchi wazingatie kanuni bora za ujenzi ili nyumba ziweze kustahimili majanga kama haya. Pia wale wanaoishi maeneo hatarishi wanapaswa kuhama mara moja kabla hawajakumbwa na maafa,” amesisitiza.
Katika tukio hilo, Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amekabidhi msaada wa Sh45 milioni, tani 10 za saruji na magodoro 20, ili kusaidia juhudi za Serikali za kuwarejeshea waathirika makazi yao.

“Tuliona ni muhimu kuwa sehemu ya juhudi za kurejesha matumaini na faraja kwa waathirika wa maafa haya. Tunaamini mchango huu utasaidia kurudisha hali ya kawaida kwa wale walioathirika,” amesema Uhadi.
Aidha, amesema mgodi huo unaendelea kushirikiana na wadau wengine ili kuhamasisha michango zaidi kwa lengo la kuboresha makazi ya wananchi walioathiriwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema zaidi ya watu 1,220 waliathirika kutokana na maafa hayo, ikiwemo kupoteza maeneo yao ya biashara.
Amesema jumla ya kata 10 ndani ya Manispaa ya Musoma zilipata athari, lakini Serikali imechukua hatua kubwa kurejesha mazingira ya waathirika katika hali ya kawaida.
Mmoja wa waathirika, Lazaro Chiguma amesema, “hali ilikuwa mbaya sana, lakini tunashukuru tumefikiwa kwa haraka na kupatiwa mahitaji muhimu. Waathirika wote tulipatiwa malazi, chakula na mahitaji muhimu wakati hatua nyingine zikiendelea,” amesema Chiguma.