Simbachawene: Madai ya Chadema hayatekelezeki

Dodoma. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiendelea kutangaza ajenda yake ya ‘No Refomrs, No Election’, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema madai ya chama hicho  kutaka katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hayatekelezeki kwa kipindi kilichobaki kuelekea Oktoba mwaka huu.

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 17, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita jijini Dodoma.

Amesema utawala bora ni utawala unaozingatia sheria na Rais Samia Suluhu Hassan ameleta falsafa ili Watanzania waiishi ya 4R ambayo ni maridhiano, maelewano, kuvumiliana na kuendelea mbele. “Tusahau yaliyopita tuendelee mbele.

Amesema falsafa hiyo imeleta mambo makubwa nchini ikiwamo kufanya marekebisho ya sheria za uchaguzi na sheria ya vyama vya siasa ambayo ni makubwa.

Pia, wamebadilisha sheria na kuunda tume huru inayojitegemea ambapo mawazo yalitolewa na vyama vyote vya siasa mchakato ambao waziri huyo alishiriki.

Amesema kutokana na mawazo yaliyotolewa na  kamati ya vyama vyote vya siasa ndiyo iliyosababisha kutengenezwa sheria ambayo ilipitishwa bungeni na wakakubaliana na tukanyamaza kimya, wakasema tunaenda kwenye uchaguzi na kama kungekuwa na mapungufu yangekuja baada ya uchaguzi huu.

“Kwamba pamoja na marekebisho haya mbona sasa hatuoni kitu ambacho kimebadilika lakini hatujaenda kwenye uchaguzi ndiyo tunaanza, lakini wapo wengine ambao wamesema hawashiriki uchaguzi siyo kazi yangu kuwataka washiriki kwa sababu ni haki ya kikatiba.”

“Lakini msingi na jambo la maana hapa ni je, mawazo yao hayo yanatekelezeka kwa kipindi hiki na kama yanatekelezeka yana gharama kiasi gani kwa kuangalia muda, kuwashirikisha wananchi ili kuwapatia haki ya kuwashirikisha kwa sababu jambo linalogusa katiba haliwezi kuwa ajenda ya kikundi cha watu, haliwezi kuwa ajenda ya CCM peke yake au ajenda ya chama fulani peke yake ni lazima liwe ajenda ya Watanzania wote,”

 “Je, katika kipindi hiki ambacho katiba yetu inasema uchaguzi ni Oktoba tunaweza tukayafanya hayo yote ya kuwashirikisha wananchi wote kwa sababu ule mchakato wa katiba mpya ile ya wakati ule tulichukua mwaka mzima sasa tunaweza tukafanya hayo? Ni dhahiri mtu anapodai kitu ambacho hakiwezekani unajiuliza dhamira yake ni nini?” amesema Simbachawene.

Amesema uchaguzi chini ya falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya maridhiano, maelewano na wengine katika mchakato huu wa kisiasa ni vizuri wakatafakari hekima, busara na falsafa hii ili waweze kuitendea haki nchi yetu kwa sababu mwisho wa siku masilahi yanayoangaliwa hapa ni ya Watanzania kwa ujumla wao na siyo ya kikundi cha watu.

“Tuna watoto, tuna kinamama, mama zetu wapo vijijini kule tukianza hekaheka hapa hakuna atakayebaki na ni kweli inatulazimu tuingie kwenye hekaheka hizo? Ni lazima sana tuingie kwenye hekaheka? Ukijiuliza busara yako itakueleza ushirikije kwenye uchaguzi na ubaya wa kudai kisichotekelezeka katika mazingira hayo,” amesema.

Wakati huohuo amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwashughulikia madereva wa Serikali wanaotumia magari ya Serikali kubebea mizigo yao binafsi na kuyatumia kwenye maeneo ya starehe.

Amesema kuna baadhi ya madereva wa Serikali ambao wanatumia magari hayo vibaya kwa kuzidisha uzito barabarani kuliko uwezo wa na iwapo watakamatwa na askari wa usalama wa barabarani wawashughulikie binafsi.

Amesema madereva wa magari ya Serikali ni lazima wazingatie sheria na kanuni zinazoongoza na siyo wayatumie kwa masilahi yao binafsi.

“Kama amebeba mkungu mmoja wa ndizi hiyo haina shida na mizigo midogomidogo lakini kubeba mizigo mpaka gari linalemewa washughulikiwe wao binafsi,” amesema Simbachawene

Kuhusu suala la ajira serikalini Simbachawene amesema hakuna Serikali duniani inayoajiri watu wake wote, na kuitaka sekta binafsi kuwezeshwa ili itoe ajira kwa wananchi na kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa kuajiri au kujiajiri wao wenyewe baada ya kumaliza masomo yao

Amesema sekta binafsi nchini ndiyo mwarobaini wa kumaliza tatizo la ajira kwa kuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri watu wote bali huwa inaajiri kutokana na uhitaji uliopo.

Amesema ushindani kwenye ajira za utumishi wa umma ni lazima kwa sababu nafasi ni chache na zinapatikana kwa ushindani, hivyo wanaoomba ajira serikalini ni lazima washindanishwe kwa kufanyiwa usaili.

Amesema usaili umewawezesha kuwapata watumishi wa umma wenye sifa baada ya kuwasaili, kwani kuna wengine hawana sifa za kuwa watumishi wa umma kutokana na haiba yao na mwonekano wao.

“Kuna mtu kwenye usaili wa kuandika amepata asilimia 100 lakini kwenye usaili wa mahojiano anafeli kwa sababu mtu anaomba nafasi ya kuwa mwalimu lakini amevaa suruali imechanika kwenye magoti, nywele amezisokota, mwingine unamwona kabisa anatumia pombe kali na mwingine anakuja amevaa tisheti (fulana) sasa huyu anakuwa hana haiba ya ualimu inayotakiwa, ukimuajiri mtu kama huyu anakwenda kufundisha nini?” amesema Simbachawene.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *