Ridhiwan aongoza mazishi ya Mama Karia

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana wenye ulemavu na makundi maalumu, Ridhiwani Kikwete, jioni ya leo Alhamisi, ameongoza waombolezaji katika mazishi ya mama mzazi wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia.

Janeth Abdallah, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana Jumatano na amezikwa jioni ya leo katika makaburi yaliyopo eneo la Bombo jijini Tanga.

Akizungumzia mbele ya waombolezaji nyumbani kwa Rais Karia Mtaa wa Bombo jijini Tanga, Ridhiwani amesema kuondokewa na mzazi ni uchungu usioelezeka.

“Kwa niaba ya serikali nakupa pole Karia na familia kwa ujumla kwa kuondokewa na mama mzazi, niwaombe muwe na subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” amesema Ridhiwani.

Mbali ya Ridhiwani, mazishi hayo yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ ambaye amesema wanamichezo nchini wapo pamoja na familia ya Rais Karia katika kuomboleza msiba huo.

MwanaFA amesema wizara inauthamini mchango wa Karia katika kuendeleza soka nchini na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla na baada ya kupata taarifa za kifo cha mama mzazi huyo wa Karia, imemtuma kuhudhuria mazishi hayo.

“Kama Naibu Waziri na Mbunge wa Jimbo la Tanga, Karia kwangu ni kaka na kiongozi ninayemthamini jitihada zake za kuendeleza soka Tanzania….Mungu awape moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” amesema MwanaFA.

Ibada ya mazishi ya mama Janeth Abdallah imeongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Sabato Usharika wa Kana jijini Tanga, Henry Mnango aliyewataka waombolezaji kutafakari kuhusu kifo.

“Waombolezaji tuliohudhuria mazishi haya, tujipe wasaa wa kutafakari kuhusu kifo, tulikuwa tukizungumza naye mama yetu juzi tu, lakini leo tunamzika, tutafakari sana kuhusu kifo,” amesema Mchungaji Mnango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *