
KOCHA wa Yanga, Miloud Hamdi avunja ukimya kuhusu kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama akisema kwa sasa gari ndo limewaka na wala hana presha ya kuchagua nani wa kuanza kikosini.
Chama aliyesajiliwa na Yanga msimu huu kutoka Simba, aliyoitumikia kwa miaka kama Simba tangu alipoua Msimbazi akitokea Power Dynamos ya Zambia, ameamua kutumika kwa muda mrefu katika kikosi cha Hamdi na juzi alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 8-1 wa mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Stand United iliyopo Ligi ya Championship.
Kauli ya Hamdi imekuja saa chache baada ya mechi hiyo na kuzima zile tetesi kwamba kiungo huyo Mzambia hana furaha Yanga kutokana na kukosa namba mbele ya mafundi wenzake waliopo kikosini.
Chama alitua Yanga akikuta wanaocheza kwenye nafasi anayoimudu ikiwa na mafundi wa zamani wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast, yaani Pacome na Aziz KI mbali na Maxi Nzengeli kutoka DR Congo.
Aziz msimu uliopita aklikuwa moro akimaliza kama Mfungaji Bora wa Ligi Kuu akiwa na mabao 21, huku Pacome na Maxi wote wakimnuka aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi, hali iliyompa wakati mgumu Chama na hata Gamondi alipoondoka alikosa nafasi chini ya Sead Ramovic.
Hata hivyo, baada ya kocha Hamdi kutua Yanga, angalu kwa sasa Chama ameanza kupata nafasi muda mwingi katika kikosi cha kwanza akipishana na Pacome na Aziz kukaa benchi na kocha huyo amefunguka sababu ya kumuamini mchezaji huyo.
Rekodi zinaonyesha tangu Hamdi aanze kazi ya kukiongoza kikosi hicho katika mechi nane, huku Chama akianzishwa katika kikosi cha kwanza katika mchezo wa kwanza dhidi ya JKT Tanzania ulioisha kwa suluhu na katika jumla ya mechi 25 za Yanga, kiiungo huyo ametumika mechi 18 kwa dakika 723, akifunga mabao matatu na asisti mbili katika Ligi Kuu mbali na yale ya Kombe la Shirikisho (FA).
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Hamdi alisema ni bahati kubwa kwake kuwa na kikosi chenye wachezaji wenye ubora wa hali ya juu hasa eneo la kiungo na kufafanua kwa nini anampa nafasi Chama.
Hamdi alisema, ingawa watu wanaona kama Chama, hapati muda wa kucheza, ila bado ni kiungo bora ndani ya Yanga na anahitajika na kuheshimika.
“Yanga ina mechi nyingi na zote watacheza, sio Chama tu anayeanzia benchi, wakati mwingine hata Aziz KI na Pacome, ila haina maana kwamba wameshindwa kucheza,” alisema Hamdi na kuongeza;
“Mabadiliko yao yanatokana na mzunguko, lakini pia kuwapumzisha wachezaji bila kusahau maamuzi ya kimbinu kutokana na mechi husika. Uwepo wa viungo hawa na wengine ni faida kwa timu, kwani tuna uhakika wa kubadilika kimbinu wakati wowote, kulingana na mpinzani tunaekutana nae.”
ISHU YA MKATABA
Chama ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia Yanga, mwisho wa msimu huu kama hataongeza basi ataingia kwenye mastaa watakaokuwa huru.
Lakini kupitia Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, kiungo huyo wiki kadhaa zilizopita alikwenda kugonga hodi kwa mabosi wake wa zamani, ila walimuwekea ngumu kwa sababu hawakufurahishwa na alivyoondoka msimu uliopita.
Mwanaspoti linafahamu kuwa, hivi karibuni Yanga imemuita Chama mezani kujadiliana nae, juu ya uwezekano wa kumuongeza mkataba mpya, huku mazungumzo ya pande hizo mbili yakiendelea, huku timu ikijiandaa kwenda Manyara kwa ajili ya mechi ya duru la pili dhidi ya Fountain Gate.
Katika mechi ya kwanza, Fountain ilifumuliwa mabao 5-0 na kumfukuzisha kazi kocha Mohammed Muta na kuletwa Mkenya Robert Matano anayedaiwa anajiuguza kwa sasa na timu kusimamiwa na msaidizi, Amri Said na wikiendi hii atakuwa na kazi ya kulipa kisasi kwa watetezi hao wanaoongoza Ligi.