AKILI ZA KIJIWENI: Bao la Mbeya City limpe somo Chamou

MUDATHIR Said alipiga bao kali sana dhidi ya Simba kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la FA lakini bahati mbaya bao lake halikuisaidia timu yake na ikajikuta ikichapwa mabao 3-1.

Lile bao limetukosha sana hapa kijiweni kwa vile mfungaji alionyesha uwezo binafsi na ujasiri wa kuwapindua mabeki wawili wa kati wa Simba, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue kisha akapiga kombora kali lililoingia wavuni.

Sio kila mchezaji wa hizi timu zetu za madaraja ya kawaida au ya chini anaweza kuwa na utayari wa kufanya kama ule wa Mudathir hivyo kwa hicho alichokifanya jamaa anastahili maua yake maana sio kila mmoja anaweza kufanya hivyo.

Hata hivyo, lile ni bao ambalo Simba inapaswa kushukuru sana kuona ikifungwa hasa katika kipindi hiki inachojiandaa na mechi mbili ngumu za nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Bao la Mbeya City kwa namna hapa kijiweni tulivyolitazama na kulichambua, Chamou Karaboue amehusika kwa kiasi kikubwa kutokana na makosa aliyoyafanya kama beki wa kati.

Kwanza hakuwa katika nafasi aliyotakiwa kuwepo wakati mpira ule unatua hadi Abdulrazack akalazimika kwenda kumsawazishia kosa lake hilo jambo ambalo lilikuwa faida ya kwanza kwa Mudathir kwa vile aliongezeka hali ya kujiamini kwa kubaki na mlinzi mmoja.

Kosa la pili likawa namna Chamou alivyoenda kutoa msaada kwa Hamza kwa vile badala ya kuilinda nafasi ambayo ilikuwa wazi, yeye akataka kukaba uelekeo uleule ambao beki mwenzake tayari alikuwa anataka kufanya jambo hilo kwa Mudathir.

Hakutakiwa kufanya vile sababu Hamza alishafanikiwa kumzibia goli Mudathir hivyo ilikuwa lazima mshambuliaji ajaribu kugeuka katika upande ambao ulikuwa wazi na ndio ulitakiwa ulindwe na Chamou Karaboue ambaye hakufanya hivyo.

Makosa kama hayo Karaboue hapaswi kuyafanya kwa vile Simba ipo kwenye mashindano makubwa ambayo yanaikutanisha na wachezaji wazuri wanaojua kutumia nafasi na uzembe wa wachezaji wa timu pinzani.

Yeye ni mchezaji wa kigeni anapaswa kuhakikisha anakuwa darasa zuri kwa wazawa na sio kinyume chake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *