AZAM FC inaomba Mungu aijaalie ipate tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa msimu ujao, licha ya ushindani inaopata kutoka kwa Singida Black Stars hapo kwenye nafasi ya tatu ambako wapo.
Ligi ndio tumaini pekee lililobakia kuipeleka Azam kimataifa kwani tayari imeshatolewa katika Kombe la TFF ambalo mshindi wake anapata tiketi ya kushiriki moja kwa moja Kombe la Shirikisho Afrika.
Hivyo kiuhakika, Azam inatakiwa imalize katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ili icheze Afrika msimu ujao vinginevyo ikiwa ya nne basi inatakiwa iombee bingwa wa Kombe la TFF awe Yanga, Simba au Singida Black Stars.

Kumaliza katika nafasi ya tatu sio kibarua rahisi kwa Azam na kocha Rachid Taoussi ana kazi ngumu ya kufanya kuhakikisha wanamaliza hapo kwani wana ushindani mkubwa kutoka kwa Singida Black Stars.
Kazi nyingine ngumu ambayo Taoussi anayo ni mchakato wa usajili wa kuimarisha kikosi chake msimu ujao kulingana na upungufu ulioonekana katika michezo ambayo imecheza msimu huu.
Sisi hapa kijiweni hatumuingilii kocha Taoussi maana yeye anajua kuliko sisi lakini mpira ni mchezo wa wazi kuna vitu tutamshauri kwa namna tulivyoiona Azam.
Taoussi aongeze mabeki kama wawili hivi wa kati wa daraja la juu ambao wataibadilisha timu badala ya kutegemea waliopo lakini pia achukue kipa mmoja wa hadhi ya nyota tano kutoka nje ya nchi kama ataachana na Mohamed Mustapha.
Pale katika kiungo apate mmoja wa kigeni wa kulinda na mwingine wa kushambulia kisha aiambie timu ijilipue kwa kusajili straika wa daraja la juu ambaye ataihakikishia zaidi ya mabao 15 katika mashindano yote kwa msimu.
Tunajua mchakato wa usajili sio kazi rahisi lakini Taoussi kwa vile ni mtaalam na ana uzoefu wa kutosha, atafanikiwa kulifanyia kazi hilo.