
Simba tayari ipo visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, huku mastaa wanne wa klabu hiyo wakibeba matumaini ya kuvuka salama katika hatua hiyo ili kutinga fainali ya michuano hiyo ya CAF.
Wekundu hao watavaana na Stellenbosch Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, uliopo Unguja kabla ya kurudiana nao Aprili 27 jijini Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa jumla atavuka kwenda fainali kusubiri kucheza ama na RS Berkane ya Morocco au CS Constantine ya Algeria.
Wakati timu ikiwa imewasilia Zanzibar jana asubuhi tayari kwa mchezo huo wa mkondo wa kwanza, mastaa wanne akiwamo kipa Moussa Camara ndio silaha kubwa zinazoweza kuwa chachu kwa Simba kufanya vyema katika mechi hizo mbili za nusu fainali ya Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch.
Namba walizonazo wachezaji hao kupitia mechi za nyuma zilizopigwa na Simba ndizo zinazowabeba mbele ya timu hiyo ya Sauzi inayoshiriki michuano hiyo ya CAF kwa mara ya kwanza na kushtua kwa kuwavua ubingwa waliokuwa watetezi, Zamalek ya Misri.
Katika mechi nane ambazo Simba imecheza kuanzia hatua ya makundi hadi robo fainali, kipa Camara, mawinga Kibu Denis na Elie Mpanzu pamoja na kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua ndio wamechangia kwa kiasi kikubwa kuifikisha Simba katika nusu fainali na wanaweza kuibeba zaidi ikiwa watalinda au wataongeza ubora wao uwanjani dhidi ya Stellenbosch.
Kipa Camara, aliokoa mikwaju miwili ya penalti katika mechi ya marudiano ya robo fainali dhidi ya Al Masry pia kabla ya hapo aliokoa penalti moja katika muda wa kawaida kwenye mechi ya makundi hidi ya Onze Bravos ya Angola.
Camara pia katika mechi hizo nane zilizopita za Simba kwenye mashindano hayo ameokoa michomo 16 ikiwa ni wastani wa hatari mbili kwa mchezo na haishangazi kuona akishika nafasi ya tatu katika orodha ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao (clean sheet) akifanya hivyo katika michezo minne.
Licha ya kuichezea Simba mechi tano tu kwenye mashindano hayo kwa vile alisajiliwa katika dirisha dogo la usajili, winga Elie Mpanzu amekuwa na matokeo chanya kwa Simba ndani ya muda mfupi alioitumikia.
Mpanzu ameshahusika na mabao mawili katika mechi hizo tano alizoichezea Simba, akifunga moja na kutoa asisti moja ya bao, pia anashika nafasi ya pili katika chati ya wachezaji waliokokota mpira kwa ukamilifu kwenye mashindano hayo, akiwa na wastani wa kufanya hivyo mara 3.6 kwa mechi.
Kibu ndiye kinara wa Simba kwa ufungaji kuanzia hatua ya makundi akifunga mabao matatu lakini pia ndiye anayeongoza katika timu hiyo kwa kuwa na wastani mzuri wa kupiga mashuti yanayolenga lango kwa usahihi ambapo kwa mchezo ana wastani wa shuti 1.3.
Takwimu zinaonyesha kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua ndiye kinara wa kutoa asisti nyingi za mabao ndani ya Simba akifanya hivyo mara mbili huku akishika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo kiujumla na amefunga mabao mawili.
Katika utengenezaji wa nafasi Ahoua ndiye mchezaji hatari zaidi wa Simba kwani amefanya hivyo mara 19, akishika nafasi ya pili katika chati ya mashindano hayo na katika nafasi hizo 19, nafasi za hatari zaidi ni nne.
Winga wa zamani wa Simba, Uhuru Selemani alisema kuwa ubora wa kikosi kizima cha Simba unaifanya iwe na nafasi nzuri ya kuitoa Stellenbosch na sio hao wanne pekee.
“Hao wanne ni mfano tu wa namna Simba ilivyo vizuri lakini kiujumla Simba ina wachezaji bora na wanaoweza kuamua matokeo hata ya mechi ngumu. Angalia mfano wa safu ya ulinzi ambavyo imekuwa ikicheza vizuri na wengineo,” alisema Uhuru na kuongeza;
“Mimi nina imani Simba itafanya vizuri dhidi ya ile timu ya Afrika Kusini ambayo haina uzoefu sana kulinganisha na Simba.”