Bei ya mafuta: Nafuu kwa watumiaji, kilio kwa wazalishaji

Katika siku za hivi karibuni, soko la mafuta duniani limejikuta kwenye mtikisiko mkubwa unaosababishwa na vuta nikuvute ya kisiasa kati ya mataifa makubwa, mabadiliko ya kiuchumi duniani, na mikakati mipya ya Jumuiya ya Nchi Wazalishaji wa Mafuta (OPEC+).

Kushuka kwa kasi kwa bei ya mafuta ghafi duniani kumeibua wasiwasi wa mdororo wa kiuchumi katika baadhi ya mataifa, huku nchi zisizozalisha bidhaa hiyo zikicheka kutokana na unafuu utakaopatikana.

Kwa nchi kama Tanzania, hali hii ni neema. Uagizaji wa mafuta kwa bei ya chini unapunguza gharama za usafirishaji na uzalishaji, hali ambayo inaweza kupunguza mfumuko wa bei na kuleta unafuu kwa wananchi.

Kadiri bei ya mafuta inavyoshuka, gharama za kusafirisha bidhaa, kuendesha viwanda, na hata uzalishaji wa chakula hupungua. Hii ni fursa ya kiuchumi kwa nchi za waagizaji kama Tanzania kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuongeza akiba ya taifa.

Hofu kuhusu athari za vita vya kibiashara katika ukuaji wa uchumi duniani na mahitaji ya mafuta kumesababisha bei ya mafuta kuporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 ndani ya wiki moja hadi kufikia kiwango cha chini kabisa katika kipindi cha miaka minne.

Sehemu kubwa kuporomoka kwa bei ya mafuta duniani kulianza Aprili 02, 2025 baada ya Rais Donald Trump kutangaza ushuru mkubwa kwa bidhaa zinazoingia katika taifa hilo namba moja kwa uchumi duniani.

Siku moja tu baada ya tangazo la Trump, kundi la OPEC+, linalojumuisha mataifa 22 wazalishaji wa mafuta likiongozwa na Saudi Arabia na Urusi, lilitangaza mpango wa kuongeza uzalishaji kuanzia Mei.

Hii ilikuwa ni kinyume na matarajio ya wengi, kwani kwa zaidi ya muongo mmoja kundi hilo limekuwa likidhibiti uzalishaji ili kudumisha bei ya juu.

Tangu wakati huo, bei za mafuta ghafi zilipungua kutoka Dola 71.7 (Sh193,139) kwa pipa hadi kufikia Dola 60 (Sh161,623) jana, Aprili 16. Hata hivyo, katikati ya kutunishiana misuli kati ya Marekani na China bei ilidondoka hadi Dola 55.4 (Sh149,231) Aprili 9 kabla haijaanza kuimarika kidogo.

Nchi kama Tanzania, Uturuki, India, Pakistan, Morocco na sehemu kubwa ya Ulaya ambazo hutegemea uagizaji wa mafuta zinatarajiwa kunufaika na kushuka kwa bei ya mafuta ghafi.

Lakini nchi zinazouza mafuta, zikiwemo zile za Ghuba, Nigeria, Angola, Venezuela na kwa kiasi fulani Brazil, Colombia na Mexico zitahisi maumivu ya kupoteza mapato ya fedha za kigeni, wamesema wawekezaji.

“Watakaoathirika watapata pigo kubwa zaidi kuliko faida wanazopata waagizaji,” anasema Thomas Haugaard, Meneja wa mfuko wa uwekezaji wa Janus Henderson Investors wa nchini Marekani.

Haugaard anaongeza: “Mauzo ya mafuta mara nyingi huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye mapato ya Serikali, jambo ambalo huathiri hatari za mikopo”.

Kicheko kwa Tanzania

Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji (Ewura), uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi uliongezeka kwa asilimia 12.1 kutoka lita bilioni 8.23 zilizoagizwa Mwaka wa Fedha 2022/23 hadi lita bilioni 9.22 zilizoagizwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24.

Kulingana na Ewura, sehemu kuu za biashara zinazotumia bidhaa za mafuta ni usafirishaji, viwanda, ujenzi, uchimbaji wa madini, kilimo na anga, hivyo kuna nafuu kubwa gharama katika uendeshaji na huduma za maeneo hayo.

Ukiachana na kiwango kinachosafirishwa kwenda nje ya nchi, katika Mwaka wa Fedha 2023/24, jumla ya lita bilioni 4.63 za mafuta zilitumika, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4.2 ikilinganishwa na lita bilioni 4.44 zilizotumika Mwaka wa Fedha 2022/23.

Wastani wa bei ya mafuta ghafi katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 ilikuwa Dola za Marekani 84.19 kwa pipa, ambayo ni pungufu ya asilimia 2 ikilinganishwa na wastani wa bei ya mafuta ghafi ya Dola za Marekani 86 kwa pipa katika Mwaka wa Fedha wa 2022/23. Sababu kuu ya kupungua kwa bei ni uzalishaji wa ziada kuliko mahitaji.

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24, wastani wa bei za rejareja za mafuta jijini Dar es Salaam ulikuwa Sh3,166 kwa lita ya petroli, Sh3,128 kwa lita ya dizeli na Sh3,030 kwa lita ya mafuta ya taa, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 kwa petroli, upungufu wa asilimia 2 na 5 kwa dizeli na mafuta ya taa, mtawalia ikilinganishwa na wastani wa bei ya mafuta katika Mwaka wa Fedha 2022/23.

Hata hivyo, kwa kawaida Tanzania hutumia mafuta yaliyoagizwa miezi miwili iliyopita, hivyo nafuu yoyote ya mwenendo wa bei ya mafuta duniani iliyoshuhudiwa mwezi huu itaonekana kuanzia Juni, 2025.

Mchambuzi wa masuala ya fedha, Innocent Baniko anasema manufaa ya kupungua kwa bei ya mafuta Tanzania yanaweza kuonekana iwapo Shilingi itaendelea kuwa imara dhidi ya fedha za kigeni, tofauti na hivyo nafuu hiyo haitawafikia wananchi.

“Hata mwezi huu Ewura ilisema sababu ya ongezeko la bei ya mafuta ni viwango vya kubadilishia fedha, hivyo hata faida za mwenendo wa bei ya sasa itatokana na uimara wa sarafu yetu, ikiwa siyo imara hatutapata kitu,” anasema Baniko.

Hata hivyo, uwezekano wa kicheko cha mafuta kuonekana Tanzania bado ni mkubwa, kwani Naibu Gavana wa BoT, Dk Yamungu Kayandabila anayesimamia uchumi na sera za fedha anasema tathimini yao inaonyesha kuwa kwa mwaka 2025 gharama ya mafuta haitazidi Dola 70 (Sh188,560) kwa pipa moja.

Dk Kayandabila pia anasema Shilingi ya Tanzania inatarajia kuimarika ifikapo mwishoni mwa waka huu kutokana na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni linalotarajiwa kwa siku zijazo.

“Tunatarajia Shilingi kuimarika sawa na ongezeko la mapato ya fedha za kigeni. Hadi Desemba tutalala usingizi na mvi zitapungua,” anasema Dk Kayandabila wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC).

Wengine maumivu

Angola ilitakiwa kulipa dola milioni 200 wiki iliyopita baada ya JPMorgan kutoa ombi la malipo ya dhamana (margin call) kutokana na mkataba wake wa swap wa faida ya jumla (total return swap) wa Dola 1 bilioni (Sh2.69 trilioni) lakini huenda likaathiriwa na hali iliyopo.

Mkataba huo wa swap ni mkopo uliotolewa na mkopeshaji huyo Desemba mwaka jana, ukiungwa mkono na dhamana ya hati fungani za Angola za dola.

“Mazingira ya sasa yameathiri soko la bidhaa na Eurobond za masoko yanayoibukia, ikiwemo kiwango cha biashara cha Eurobond za Angola, na kumesababisha ombi la margin call. Angola ilitimiza wajibu wake kwa wakati na kwa fedha taslimu,” wizara hiyo iliiambia Reuters siku ya Jumatatu.

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linalitambua deni la Angola kuwa kwenye hatari kubwa ya matatizo ya ulipaji, lakini serikali ya Angola imesema mwenendo wa deni la taifa uko imara na kwenye njia thabiti.

Kwa upande wa Nigeria, kushuka kwa bei ya mafuta kwa muda mrefu kunaweza kudhoofisha maendeleo ya hivi karibuni ya mageuzi ya kiuchumi, na hata kuyarejesha nyuma, walisema wachambuzi.

Mafuta huchangia karibu asilimia 90 ya mauzo ya nje ya Nigeria na mapato ya mauzo ya mafuta yalitarajiwa kugharimia asilimia 56 ya bajeti ya mwaka huu. Serikali ilikadiria bei ya mafuta kuwa dola 75 (Sh202,028) kwa pipa kwenye bajeti ya 2024, lakini imelazimika kubadili mpango wake.

“Tunarudi mezani kuangalia bajeti yetu upya,” alisema Waziri wa Fedha, Wale Edun wakati akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita.

Wiki hii bei ya mafuta ya Urals kutoka Urusi iliporomoka hadi dola 53 (Sh142,767) kwa pipa, hali ambayo inaweza kulazimisha Urusi “kudhoofisha sarafu yake, ruble, kwa kiwango kikubwa,” alisema Chris Weafer, mshauri wa uwekezaji ambaye amefanya kazi Urusi kwa zaidi ya miaka 25.

Urusi imekuwa ikitegemea mapato ya mafuta kufadhili bajeti ya matumizi ya kijeshi, hasa baada ya kuanza kwa vita dhidi ya Ukraine.

Hata hivyo, wazalishaji mafuta kama Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu wanaweza kustahimili hali hii vyema zaidi kutokana na akiba kubwa, madeni madogo na hatua fulani za mwelekeo wa tofauti kiuchumi, walisema wachumi.

Hata hivyo, kushuka kwa mapato kunaweza kuathiri uwezo wao wa kutumia fedha kwenye miradi mipya, ikiwemo Saudi Arabia, ambayo ni kiongozi halisi wa OPEC.

“Kushuka kwa bei ya mafuta ni chanya kwa waagizaji wa mafuta, ingawa haiwezekani kufidia changamoto kubwa kutoka kwenye vita vya kibiashara na hatari kubwa za kushuka kwa uchumi,” alisema Monica Malik, Mchumi mkuu katika Benki ya Biashara ya Abu Dhabi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *